Na Mwandishi Wetu, Arusha
 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Arusha, Paul Christian Makonda, ameridhishwa na maboresho yanayoendelea katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center inayotoa huduma kwa ushirikiano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, ALMC–JKCI Arusha.

Maboresho hayo yanafanyika kwa uwezeshaji wa Global Medicare, kwa lengo la kuongeza ubora wa huduma za afya, kuboresha mazingira ya matibabu, kuimarisha utalii tiba na kuiandaa hospitali kutoa huduma zinazokidhi viwango vya kimataifa kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2027.

“Lengo kubwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kabisa na katika mazingira mazuri. Vilevile tunataka kuimarisha utalii tiba na kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya AFCON 2027,” alisema Mhe. Makonda.

 Makonda alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya na kuruhusu taasisi za kibingwa kama JKCI kupanua huduma zake hadi mikoani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa JKCI ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dkt. Peter Kisenge, alisema maboresho yanayoendelea yanalenga kuibadilisha ALMC–JKCI kuwa kituo cha kisasa cha huduma za kibingwa chenye mazingira rafiki kwa wagonjwa.

Dkt. Kisenge alisema lengo ni kuhakikisha mgonjwa anapofika hospitalini anakutana na mazingira yenye usafi, utulivu, faraja na huduma zinazofanana na zinazopatikana katika hospitali kubwa za kimataifa.

“Tunataka mgonjwa anapokuja hapa asiingie katika mazingira yanayomwongezea hofu. Tunataka akute hospitali yenye mazingira mazuri, tulivu na yenye huduma zinazompa faraja,” alisema Dkt. Kisenge.

Kwa mujibu wake, skrini moja itaonyesha taarifa za wagonjwa waliopo wodini, ikiwemo mapigo ya moyo, kiwango cha oksijeni kwenye damu, shinikizo la damu na viashiria vingine muhimu vya afya.
Skrini nyingine itaunganishwa na mfumo wa Dozee, teknolojia inayowezesha mgonjwa kuendelea kufuatiliwa hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Alisema mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji, upasuaji wa kujifungua au matibabu mengine yanayohitaji uangalizi wa siku kadhaa ataweza kufuatiliwa akiwa nyumbani, huku wauguzi na madaktari wakipokea taarifa za afya yake kwa wakati.

Dkt. Kisenge alisema mfumo huo utasaidia kugundua mapema mabadiliko ya hali ya mgonjwa na kuwawezesha wataalamu wa afya kuchukua hatua kabla hali haijawa mbaya.
Alisema vyumba vya wagonjwa vitawekewa vifaa vya kisasa vya ufuatiliaji, televisheni na mifumo ya kidijitali ya kuhifadhi historia ya mgonjwa, uchunguzi, dawa na matibabu yote anayopatiwa.
Dkt. Kisenge alisema hospitali pia inaandaa wodi maalumu ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu baada ya kutoka katika chumba cha wagonjwa mahututi, inayojulikana kama High Dependency Unit.

Dkt. Kisenge alisema mashine ya Cath Lab yenye thamani ya takribani shilingi bilioni tatu inatarajiwa kuwekwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya matatizo ya mishipa ya moyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Kliniki wa ALMC–JKCI Arusha, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Dkt. Sakeh Hamisi Mwishete, alisema uongozi wa hospitali umeweka mkakati wa kuhakikisha wagonjwa wenye mahitaji tofauti wanapata huduma zinazowafaa.
Dkt. Mwishete alieleza kuwa vyumba vya VIP vimewekewa vifaa vinavyowezesha kubadilishwa haraka kuwa vyumba vya uangalizi maalumu au ICU endapo hali ya mgonjwa itabadilika.
 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mji
“Hiki ni chumba cha VIP, lakini kimewekewa vifaa maalumu. Endapo hali ya mgonjwa itabadilika, kinaweza kupandishwa hadhi na kutoa huduma za dharura au huduma zinazohitajika katika ICU bila kuchelewa,” alisema Dkt. Mwishete.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura katika ALMC–JKCI Arusha, Dkt. Farida Abdallah, alisema kitengo cha dharura kinaendelea kupokea wagonjwa kutoka Arusha, Manyara, Singida na maeneo mengine ya Kanda ya Kaskazini.

“Lengo letu kubwa ni kuhakikisha mgonjwa wa dharura anapata huduma kwa wakati ili kuzuia madhara ya kudumu au kupoteza maisha. Mimi pamoja na timu yangu tunafanya kazi saa 24 kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma za haraka,” alisema Dkt. Farida.