Dar es Salaam, 16 Julai 2026 — Kiongozi wa biashara kutoka Tanzania, Milu Kipimo, ameteuliwa kuwa Meneja wa Kanda ya Afrika wa Bolt for Business, hatua inayompa jukumu la kusimamia shughuli za huduma za usafiri wa biashara za kampuni hiyo katika masoko yote ya Afrika ambako Bolt inafanya kazi.
Kabla ya uteuzi huo, Kipimo alikuwa Meneja Mwandamizi wa Nchi, akisimamia shughuli za Bolt for Business nchini Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia na Ghana. Alijiunga na Bolt mwaka 2018 akiwa miongoni mwa wafanyakazi wa kwanza wa kampuni hiyo nchini Tanzania. Tangu mwaka 2021, ameongoza uzinduzi na ukuaji wa Bolt for Business nchini, akiiwezesha kuwa kampuni inayaoongoza kwa huduma za usafiri kwa wateja wa taasisi na makampuni.
Katika nafasi yake mpya, Kipimo atasimamia maendeleo ya biashara katika masoko yote ya Bolt barani Afrika pamoja na kukuza uwezo wa timu za ndani ili kuhakikisha kampuni na taasisi zinapata huduma zenye ubora, unyumbufu na usimamizi bora wa akaunti kupitia Bolt for Business kama mbadala wa mifumo ya kawaida ya usafiri wa kikazi.
Akizungumzia uteuzi huo, Mkurugenzi wa Kanda wa Bolt for Business, Juliano Fatio, alisema:“Tunafurahia kumkabidhi Milu jukumu la kuongoza shughuli za Bolt for Business barani Afrika. Uzoefu wake katika masoko ya Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia na Ghana utakuwa mchango mkubwa tunapoendelea kupanua huduma zetu barani na kuwahudumia wateja wetu wa biashara kwa ubunifu na ufanisi zaidi. Uteuzi huu unaonesha dhamira yetu ya kuendelea kuwekeza katika soko la Afrika.”
Kwa upande wake, Kipimo alisema:“Nimeheshimika kupewa nafasi ya kuongoza Bolt for Business Afrika. Natarajia kutumia uzoefu nilioupata katika masoko ya Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini kuimarisha ukuaji wa biashara katika bara zima, huku tukiendelea kutoa huduma bora ambazo wateja wetu wa biashara wanazitarajia kutoka Bolt Business.”
Bolt for Business ni sehemu ya dhamira ya Bolt ya kujenga miji inayoweka watu mbele kuliko magari. Huduma hiyo ilizinduliwa mwaka 2018 na huwasaidia waajiri kurahisisha usafiri wa wafanyakazi kwa safari za kila siku na shughuli za kikazi, huku ikipunguza urasimu wa malipo na madai ya marejesho ya fedha. Kufikia Desemba 2024, Bolt for Business ilikuwa inapatikana katika zaidi ya masoko 50 duniani, ikihudumia zaidi ya kampuni 50,000.


