Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Baadhi ya wananchi waliotembelea Kijiji cha Bima katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, wamepongeza uwepo wa jukwaa hilo na kuomba liendelee kuandaliwa kila mwaka.
Wananchi hao pia wameiomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kushirikisha kampuni nyingi zaidi za bima katika maonesho yajayo ili wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kupata elimu na huduma za bima katika eneo moja.
Mwaka huu, Kijiji cha Bima kilivutia zaidi ya kampuni 40 za bima zilizopata nafasi ya kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali za bima, kujipatia wateja wapya pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wateja wao.
Bi. Anita Ndimbo, mmoja wa wananchi waliotembelea Kijiji hicho, alisema utaratibu huo umeleta urahisi mkubwa kwa wananchi kufikia kampuni nyingi za bima kwa wakati mmoja na kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma wanazohitaji.
“Huu ni utaratibu mzuri sana kwani imekuwa rahisi kufikia kampuni nyingi kwa wakati mmoja na kufanya maamuzi sahihi. TIRA ina wajibu wa kufikia kampuni nyingi zaidi za bima ziwe sehemu ya utaratibu huu, huku wananchi wakihamasishwa zaidi kuhusu umuhimu wa bima,” alisema.
Kwa upande wake, Mgeni Ali alisema alifurahishwa na uwepo wa Kijiji cha Bima kwani kilimpa fursa ya kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali za bima ambazo hapo awali hakuwa akizifahamu.
“Nilikuja Sabasaba kujionea mambo mbalimbali, lakini nilipoona kuna Kijiji cha Bima nilivutiwa kuja kupata elimu. Kuna aina nyingi za bima ambazo sikuwa nazifahamu. Sasa nina uelewa wa kutosha wa kufanya maamuzi sahihi,” alisema.
Naye Suleiman Mohamed aliwataka wananchi kuondokana na dhana potofu kwamba bima ni kwa ajili ya afya pekee, akieleza kuwa zipo huduma nyingi za bima zinazolenga kulinda maisha na mali za wananchi.
“Kupitia Kijiji hiki cha Bima nimejifunza mambo mengi. Awali niliona umuhimu wa bima ya afya tu, lakini sasa nimefahamu kuwa zipo pia bima za mifugo, nyumba, biashara na nyingine nyingi,” alisema.
Kijiji cha Bima ni jukwaa la kila mwaka linaloratibiwa na TIRA kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya bima kwa lengo la kuwasogezea wananchi elimu ya bima, ushauri wa kitaalamu pamoja na huduma mbalimbali za bima katika eneo moja.
Kupitia jukwaa hilo, wananchi hupata nafasi ya kujifunza umuhimu wa kuwa na bima mbalimbali zinazolinda maisha, afya, mali, biashara na uwekezaji wao dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kujitokeza.
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi Kijiji cha Bima baada ya kumalizika kwa Maonesho ya Sabasaba, Kamishna wa Bima, Dkt. Saqware, aliyewakilishwa na Mkurugenzi wa Tafiti na Uendelezaji wa Soko wa TIRA, Bw. Zakaria Muyengi, alizipongeza kampuni za bima kwa mchango wao katika kufanikisha shughuli hiyo.
Alisema kupitia Kijiji cha Bima wananchi wengi wamepata elimu ya bima pamoja na huduma mbalimbali zilizosaidia kutatua changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo.
“Kupitia fursa hii tumeweza kutoa elimu kwa wananchi na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili. Bado tunayo kazi kubwa ya kuendelea kuwaelimisha Watanzania kuhusu masuala ya bima na umuhimu wake,” alisema.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia huduma za bima kama nyenzo muhimu ya kudhibiti vihatarishi na kujenga ustahimilivu wa kifedha kwa watu binafsi, biashara na taasisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kijiji cha Bima, Bw. Kelvin Mushi, alisema mafanikio yaliyopatikana mwaka huu yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya TIRA na kampuni mbalimbali za bima.
“Tunaamini mwakani tutafanya vizuri zaidi na kuendelea kuboresha Kijiji cha Bima ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, ambalo ndilo lengo kuu la kuanzishwa kwa jukwaa hili,” alisema, huku akiipongeza TIRA kwa kubuni mpango huo.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yalianza rasmi tarehe 28 Juni 2026 na kuhitimishwa tarehe 14 Julai 2026, yakivutia maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali za nchi kila siku.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia, kuendeleza na kuhakikisha sekta ya bima nchini inakuwa imara, yenye ushindani na inayolinda maslahi ya watumiaji wa huduma za bima.




