📌Yalenga kupunguza vifo kwa asilimia 50 ifikapo 2030
Wizara ya Ujenzi imesema inaendelea kutekeleza Mradi wa kuimarisha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA), ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu ya barabara, kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na kupunguza ajali zinazosababisha vifo, majeruhi na hasara za kiuchumi.
Wizara imeeleza kuwa kupitia mradi huo, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwa kuzingatia viwango vya usalama ambapo maboresho hayo yanajumuisha uwekaji wa alama za barabarani, taa za kuongozea magari katika maeneo muhimu, vizuizi vya usalama, pamoja na ujenzi wa njia za waenda kwa miguu na madaraja ya watembea kwa miguu katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.
Akizungumza jijini Dodoma, Juni 21, 2026, wakati wa kikao cha Kamati Maalum ya Mradi wa kuimarisha Usalama Barabarani, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema mradi huo unalenga kupunguza ajali za barabarani kwa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa usalama pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Dkt. Msonde amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa katika sehemu tatu, ikiwemo uanzishaji wa mfumo wa kisasa wa kukusanya taarifa za ajali kwa wakati halisi.
Mfumo huo utaziwezesha mamlaka husika kupata taarifa muhimu, zikiwemo eneo la ajali, idadi ya majeruhi na taarifa nyingine zitakazosaidia kuchukua hatua za haraka, kuboresha huduma za dharura na kupanga mikakati madhubuti ya kudhibiti ajali.
Aidha, mradi huo unahusisha utoaji wa mafunzo ya usalama barabarani kwa jamii pamoja na kuandaa mitaala ya elimu ya usalama barabarani itakayofundishwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo.
“Matarajio yetu ni kwamba ifikapo mwisho wa mradi huu tutakuwa tumefanikisha mambo makubwa matatu, ikiwemo kuwa na mfumo madhubuti wa taarifa za ajali na kutumia taarifa hizo kupanga mikakati ya kuzuia ajali za barabarani,” amesema Dkt. Msonde.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Usalama na Mazingira wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Musa Kashinde, amesema mkakati wa mradi huo unaendana na azma ya Serikali ya kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Mhandisi Kashinde ameongeza kuwa timu ya utekelezaji imepokea maelekezo kutoka kwa wataalamu wa mradi na imejipanga kuyatekeleza kikamilifu ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2025 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028 ambapo mbali na kuboresha miundombinu ya barabara, mradi huo pia unatoa mafunzo ya usalama barabarani kwa jamii, ikiwemo wanafunzi wa shule na vyuo, kwa lengo la kujenga utamaduni wa matumizi salama ya barabara nchini.








