Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 25, 2026 ameongoza Watanzania kuadhimisha Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa katika Uwanja wa Mashujaa, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya Taifa kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliotoa mchango wao katika kupigania kulinda mipaka ya nchi na kujitolea kwa ajili ya amani, umoja na maendeleo ya Tanzania.
Rais Samia aliwasili katika eneo la tukio na kupokelewa kwa heshima za kijeshi kabla ya kusikiliza wimbo wa Taifa pamoja na wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baadaye, Rais aliweka shada la maua kwenye Mnara wa Mashujaa ikiwa ni ishara ya heshima na kutambua mchango wa Watanzania walioweka maisha yao mbele kwa ajili ya kulinda Taifa.
Tukio hilo lilifuatwa na dakika za ukimya kuwaenzi mashujaa waliopoteza maisha wakilitumikia Taifa kwa uaminifu, ujasiri na uzalendo.
Maadhimisho hayo yamewahusisha viongozi wakuu wa Serikali, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, wanajeshi wastaafu pamoja na wananchi mbalimbali waliokusanyika kushiriki katika tukio hilo la kitaifa.
Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa imeendelea kuwa ukumbusho kwa Watanzania kuwa uhuru, amani na utulivu unaofurahiwa leo haukuja kwa bahati, bali ulipatikana kupitia juhudi, kujitolea na uvumilivu wa watu walioweka maslahi ya Taifa mbele kuliko yao binafsi.
Kupitia maadhimisho hayo, Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda tunu za Taifa, kudumisha umoja wa kitaifa na kuenzi mchango wa wale walioacha alama katika historia ya Tanzania.






