Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni, Wilaya ya Kimbiji, limesogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa elimu kwa wakazi wa Mwasonga kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, utaratibu mpya wa kuomba huduma ya umeme kupitia mfumo wa NIKONEKT JISOTI, matumizi ya Luku Janja pamoja na huduma ya MCHONGO 180.
Akizungumza leo, Julai 31, 2026, wakati wa utoaji wa elimu hiyo kwa wakazi wa Mwasonga, Kimbiji, Dar es Salaam, Meneja wa TANESCO Wilaya ya Kimbiji, Mhandisi Lukaluka Kapinga, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati.
Mhandisi Kapinga ameongeza kuwa TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya majiko ya umeme kutokana na ufanisi, usalama na urahisi wake, huku ikiendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme kwa wananchi.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya, ameelezea utaratibu mpya wa kuomba huduma ya umeme kupitia mfumo wa NIKONEKT JISOTI. Amesema mfumo huo umeboresha utoaji wa huduma kwa kurahisisha mchakato wa maombi, kuharakisha upatikanaji wa huduma na kuongeza uwazi.
Aidha, amesema kupitia mfumo huo wananchi wanaweza kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme, kufuatilia hatua za maombi na kupata taarifa mbalimbali kwa urahisi, hali inayopunguza muda wa kusubiri huduma.
Akitoa elimu kuhusu huduma ya MCHONGO 180, Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Kimbiji, Paschal Mapunda, amesema huduma hiyo imeanzishwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya shirika na wananchi.
“MCHONGO 180 ni njia rahisi na ya haraka inayowawezesha wananchi kuwasiliana na TANESCO wakati wowote wanapohitaji huduma au wanapokumbana na changamoto za umeme. Tunawahimiza wananchi kuitumia huduma hii ili kupata msaada kwa wakati,” amesema Mapunda.
Naye, Afisa Huduma kwa Wateja wa TANESCO Kimbiji, Faith Mtoi, amewahamasisha wananchi kutumia majiko ya umeme, akieleza kuwa yana ufanisi mkubwa, yanaokoa muda wa kupika, ni salama na yanachangia kulinda afya pamoja na mazingira.
Baada ya kupokea elimu hiyo, wakazi wa Mwasonga wamelishukuru TANESCO kwa kuwafikia moja kwa moja na kuwapatia uelewa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika.











