Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa taasisi ya Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Africa50 General Shareholders’ Meeting – GSM and Infra for Africa Forum) inayotegemewa kufanyika tarehe 5 na 6 Agosti, 2026 katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Center (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Washiriki wapatao 1,200 wakiwemo viongozi wa Serikali, wanahisa wa Africa50, taasisi za fedha, wawekezaji wa kimataifa na sekta binafsi wanategemea kushiriki katika mikutano hii.

Mikutano hiyo inatarajia kuipatia Tanzania fursa ya kutangaza vivutio vya utalii, uwekezaji na miradi ya kimkakati kwa lengo la kuvutia mitaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu na hivyo kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Kitaifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa ujumla, na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.

Africa50 ni taasisi ya fedha inayoshirikiana na Serikali barani Afrika kuandaa miradi hadi kufikia hatua ya kupata wawekezaji (bankable projects); na kutafuta wawekezaji kwa utaratibu wa equity investment kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi kutoka kwa wawekezaji na wafadhili wa ndani na nje ya Afrika. Lengo ni kuharakisha utekelezaji wa miundombinu yenye ubora kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Miundombinu ya kipaumbele ni pamoja na nishati, uchukuzi, elimu, afya, mawasiliano na fedha (fintech). Hivyo inategemewa mkutano utavutia wawekezaji wa kimataifa kutangaza miradi ya kimkakati kama reli ya SGR, Bandari ya Dar es Salaam, uzalishaji wa umeme, na miundombinu ya TEHAMA.