Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma
Serikali imeeleza kuwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi hakutakuwa na tija endapo hautaambatana na usindikaji, viwango bora na upatikanaji wa masoko ya uhakika, huku ikitaka taasisi zote zinazohusika na sekta hizo kuunganisha nguvu katika kujenga mnyororo kamili wa thamani.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 2,2026 na Waziri wa Fedhaa Khamis Musa Omary alipotembelea mabanda mbalimbali kwenye Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, ambapo alijionea teknolojia, bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi za Serikali pamoja na sekta binafsi.
Amesema hatua ya kuongeza uzalishaji pekee haitoshi kama bidhaa zinazozalishwa haziwezi kufikia masoko kwa ubora unaohitajika na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.
“Wadau wote wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha mnyororo mzima wa uzalishaji unaimarika, kuanzia uzalishaji wenyewe, usindikaji, upatikanaji wa mitaji, viwango vya ubora hadi bidhaa kufika sokoni,” amesema.
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya sekta za fedha, kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na taasisi nyingine za Serikali ni muhimu katika kuondoa vikwazo vinavyopunguza tija na ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti na ubunifu ili kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili wazalishaji, akisema uwekezaji huo unaweza kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa muda mrefu.
Waziri huyo pia ameeleza kufurahishwa na maendeleo ya sekta ya ufugaji wa samaki, akisema ina fursa kubwa ya kuongeza upatikanaji wa chakula chenye virutubisho na kuinua kipato cha wananchi.
Alibainisha kuwa kutokana na changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi wa asili katika bahari na maziwa, ni muhimu kuendelea kuwekeza katika ufugaji wa samaki ili kuongeza uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko.
Vilevile, aliwataka wadau wa viwango kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi matakwa ya soko, hatua ambayo itaongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Pia alitoa wito wa kutangaza zaidi bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali wa ndani ili kuongeza uelewa wa wananchi na kupanua fursa za biashara, akisisitiza kuwa ubora na uzalishaji wa kutosha ni msingi wa ushindani wa bidhaa hizo.
Akihitimisha ziara hiyo, Waziri huyo amewapongeza wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi kwa juhudi wanazoendelea kufanya, huku akieleza kuwa ushirikiano katika mnyororo mzima wa thamani ndiyo utakaowezesha sekta hizo kutoa mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.



