….Kampuni ya Betaren yaanza kuingiza mbegu bora aina ya Bombadier, Daha, Bazik na Krechet

Na Mwandishi Wetu

Ziara ya kikazi ya siku tatu aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi Juni 3 mwaka huu imeanza kulipa baada ya kampuni za kutoka nchini humo ikiwemo Betaren kuja kuwekeza kwenye mbegu za kisasa za mazao.

Kampuni ya Sky Business and Investment Company Ltd imeingia ubia na kampuni hiyo yenye asili ya Urusi ya Betaren kwaajili ya kusambaza mbegu bora za kisasa, mbolea na viuatilifu kwa wakulima Tanzania.

Aina ya mbegu ambazo kampuni hiyo imeanza kuingiza nchini ni pamoja na mbegu aina ya Bombadier, Daha, Bazik na Krechet ambazo ziko kwenye hatua za mwisho kupata kusajili.

Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la kampuni hiyo kwenye maonesho ya nane nane mkoani Dodoma, Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo alisema ujio wa kampuni hiyo kuwekeza nchini ni matokeo ya diplomasia ya uchumi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyetembelea Urusi hivi karibuni.

Alisema wawekezaji kutoka Urusi wameanza kumiminika nchini kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kampuni ya Betaren ambayo imeanza kuingiza mbebu bora za kisasa.

“Hii ni kampuni kubwa Urusi imeanza kushirikiana na wenzao wa hapa Tanzania Sky Business and Investiment na kwenye maeneo ambayo mbegu hizi zimefanyiwa majaribio tumeambiwa kuwa mafanikio ni makubwa sana,” alisema

“Kwa mbegu hizi mkulima anaweza kuvuna mara mbili ya kile alichokuwa analima awali, yaani kama alikuwa anavuna tani 50 basi kwa kutumia mbegu hizi atavuna tani 100,” alisema

Aliomba mamlaka inayohusika na usajili wa mbegu nchini kufanya mchakato wa haraka ili kumwezesha mwekezaji huyo kuendelea na shughuli zake hapa nchini ambazo zitasaidia kukuza uchumi wa wakulima na wataifa kwa ujumla.

“Tunachangamoto ya kuagiza mafuta nje ya nchi lakini kwa mbegu hizi inamaana kama zitawafikia wakulima wengi tutaweza kuzalisha kwa wingi mafuta na kuondokana na uagizaji mafuta,” alisema

“Tunatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi sasa mbegu hizi za alizeti zitaongeza uzalishaji wa alizeti na uzalishaji wa mafuta naishukuru kampuni hii kwa kuchagua kuja kuwekeza Tanzania na namshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema

Omary Issa, ambaye ni mkulima wa Alizeti Bagamoyo ambaye ametumia mbegu za Bombadier, Daha, Bazik na Krechet alisifu ubora wa mbegu hizo na kwamba zitamwezesha kuwa na kipato kuzuri.

“Mbegu hizi zimenionyesha kuwa nitakuwa na kipato kizuri kwenye mnyororo wa thamani wa bidhaa za alizeti kwasababu nitakuwa navuna mavuno mengi kwa kutumia mbegu hizi,”alisema

Mkurugenzi wa Biashara wa Sky Business and Investiment, Said Salum alisema watafanyabiashara kwa ushirikiano na kampuni hiyo ya Urusi kwa upande wa mbegu bora, mbolea na viuatilifu.

Alisema ujio wa kampuni hiyo ni matunda ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi ambapo wawekezaji hao waliona fursa mbalimbali zilizoko nchini na wameanza kuzitumia kwa kuja kuwekeza hapa nchini.

“Kwa ubia na kampuni hii ya Urusi tunawahakikishia wakulima kupata mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwaajili ya kuzalisha kwa wingi na kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu,” alisema