Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

SHIRIKA la Vi Agroforestry Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wake akiwemo Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO), limeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kuhamasisha matumizi ya kilimo misitu kama suluhisho la kuongeza uzalishaji wa chakula, kuboresha lishe, kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya John Malecelea jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkaazi wa Vi Agroforestry Tanzania, Martha Olotu, alisema shirika hilo linaendelea kuhamasisha mfumo wa kilimo unaounganisha mazao, miti na mifugo katika eneo moja ili kuongeza tija ya uzalishaji, kuboresha rutuba ya ardhi na kuongeza kipato cha wakulima.

Alisema banda la Vi Agroforestry limepokea idadi kubwa ya wakulima, wataalamu na wananchi waliotembelea kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo misitu pamoja na kuona bidhaa zinazotokana na mfumo huo, zikiwemo mbegu za asili, unga wa ubuyu, vyakula vya lishe na mazao mengine yanayoongeza thamani ya kilimo.

“Lengo letu ni kuhakikisha wakulima wanatumia maeneo madogo kwa ufanisi, wanapata mazao mengi, wanaimarisha lishe za familia zao na kuongeza kipato huku wakilinda mazingira,” alisema Olotu.

Aidha, alitangaza kuwa Vi Agroforestry linaendelea na maandalizi ya Kongamano la 11 la Kilimo Misitu, litakalofanyika mwezi Oktoba.

Abdallah Ramadhani Mkindi, ambaye ni Mratibu wa Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO) alisema

“Mimi naitwa Abdallah Ramadhani Mkindi, ni Mratibu wa Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO) sisi ni miongoni mwa wadau na wanufaika tunaofanya kazi kwa karibu na Vi Agroforestry katika utekelezaji wa mradi wa ASILI-B,” alisema na kuongeza.

“Kupitia ushirikiano huu, Vi Agroforestry imeendelea kutuwezesha kushiriki katika maonesho mbalimbali kama haya ya Nanenane, ambayo yanatupa fursa ya kukutana na wadau tofauti, kubadilishana uzoefu na kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya kilimo misitu, uhifadhi wa baionuwai na matumizi endelevu ya maliasili,” alisema.

Aidha, alisema ushirikiano huu umewawezesha kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za kilimo endelevu, kuhifadhi mbegu za asili, kulinda mazingira na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tunaamini kwamba kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, tutaweza kuleta mabadiliko chanya katika uhifadhi wa mazingira na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema .

“Kwanza, napenda kuwapongeza na kuwashukuru Vi Agroforestry pamoja na wadau wote kwa ushirikiano mkubwa katika kuhamasisha masuala ya kilimo misitu nchini kwani kupitia maonesho haya ya Nanenane, tumepata fursa ya kukutana na wananchi na kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kilimo misitu na mchango wake katika kuboresha rutuba ya udongo, kuhifadhi mazingira na kuongeza uzalishaji wa mazao,” alisema Edna Paul.

Vilevile, alisema kilimo misitu kina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa chakula kwa kaya, kuongeza kipato cha wananchi na kuwasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri sekta ya kilimo.

“Hii ni fursa muhimu sana kwa wadau kuendelea kuwafikia wananchi, kusikiliza changamoto wanazokutana nazo na kwa pamoja kutafuta suluhisho endelevu. Tunaamini kuwa kupitia elimu na ushirikiano huu, jamii itaendelea kuelewa na kutumia mbinu za kilimo misitu ambazo zitaleta manufaa kwa mazingira na maisha ya wananchi kwa ujumla,” alisema.