Na.Mwandishi Wetu
Tume ya Ushindani (FCC) imetajwa kuwa mdau muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya Watanzania kupitia elimu ya ushindani wa haki na ulinzi wa mlaji, hatua inayowasaidia wazalishaji na wafanyabiashara kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuzifanya zishindane katika masoko ya ndani na kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 7,2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, alipotembelea banda la FCC katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema elimu inayotolewa na tume hiyo imeendelea kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa ushindani wa haki, ulinzi wa mlaji na kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania.
Ameipongeza FCC kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha mazingira ya biashara, akieleza kuwa juhudi hizo zinaendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta za uzalishaji kupitia soko lenye ushindani wa haki, uwazi na fursa sawa kwa wote.
Mhe. Londo ameihimiza FCC kuendelea kutumia Maonesho ya Nanenane na majukwaa mengine kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuongeza uelewa kuhusu sheria za ushindani na ulinzi wa mlaji, akisisitiza kuwa elimu hiyo ni nyenzo muhimu ya kuongeza thamani ya mazao, kuvutia masoko mapya na kuongeza kipato cha wazalishaji.
Aidha, ametoa wito kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali kwenda kuitumia vizuri elimu iliyotolewa na FCC kuboresha uzalishaji wao, kuzingatia sheria za ushindani na kuepuka vitendo vinavyovuruga soko, akieleza kuwa hatua hiyo itachangia kujenga uchumi shindani na kuongeza mchango wa sekta za uzalishaji katika maendeleo ya taifa.








