DODOMA
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amesema Maonesho ya Nanenane ni jukwaa muhimu la kuwaelimisha wananchi kuhusu Sekta ya Madini, kusikiliza maoni yao na kupata mrejesho unaosaidia kuboresha huduma na kuongeza thamani ya sekta hiyo.
Mhandisi Swedi amesema hayo baada ya kutembelea mabanda ya Taasisi za Wizara ya Madini katika kilele cha Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma, akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika maendeleo ya sekta hiyo.
Amesema maonesho hayo yanawezesha Tume ya Madini kuwafikia wananchi moja kwa moja, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kupata maoni ambayo yanaweza kutumika kuboresha utendaji na utoaji wa huduma.
“Kila swali na hoja inayotolewa na mwananchi ni muhimu, kwa sababu inatusaidia kutambua maeneo yanayohitaji maboresho na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma,” amesema Mhandisi Swedi.
Aidha, amesema ushiriki wa wananchi katika Maonesho ya Nanenane unaimarisha ushirikiano kati ya Serikali, taasisi zinazohusika na Sekta ya Madini na jamii, sambamba na kuwawezesha wananchi kupata uelewa kuhusu huduma, fursa na shughuli mbalimbali zinazopatikana katika sekta hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Swedi ametembelea mabanda ya Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ambako amepata fursa ya kujionea huduma na shughuli zinazotekelezwa na taasisi hizo.
Amewahimiza wananchi kutumia kikamilifu fursa inayotolewa na Maonesho ya Nanenane kwa kujifunza, kuuliza maswali na kutoa maoni kuhusu Sekta ya Madini.
Pia, amewakaribisha wananchi kufika katika ofisi za Tume ya Madini na taasisi nyingine zinazohusika na sekta hiyo ili kupata ufafanuzi na huduma zaidi kuhusu masuala ya madini.







