▪️ Lengo ni kuchukua hatua kwa wanaoitumia vibaya
▪️ Waziri Mavunde aelekeza RMOs kufanya ukaguzi wa mara kwa mara
▪️ Mchango wa wachimbaji wadogo kwenye uzalishaji madini wakua
▪️ Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kutupia jicho kwenye maabara za upimaji sampuli za madini
*DODOMA
Serikali imeandaa operesheni maalum ya kukagua utekelezaji wa mikataba ya msaada wa kiufundi katika shughuli za madini, ikiwa ni hatua ya kuangalia utekelezaji wake kwa mujibu wa sheria na kuchua hatua stahiki,kulinda maslahi ya wamiliki wa leseni na kuhakikisha mikataba hiyo haitumiki kuwanyima mapato na haki zao.
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema hayo mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya sekta ya madini nchini katika uongezaji thamani madini ndani ya nchi.
Mavunde ameelekeza Maafisa Madini Wakazi (RMOs) kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa utekelezaji wa mikataba hiyo katika maeneo ya migodi, ili kubaini changamoto mapema na kuchukua hatua dhidi ya watakaobainika kutumia mikataba ya msaada wa kiufundi kuwanyonya wamiliki wa leseni.
Amesisitiza kuwa mikataba ya msaada wa kiufundi inapaswa kuongeza uzalishaji, tija na ufanisi katika shughuli za madini, badala ya kuwa chanzo cha migogoro au kupunguza manufaa anayopaswa kupata mmiliki wa leseni.
Akizungumzia uzalishaji wa dhahabu, Mavunde amesema Tanzania huzalisha wastani wa takribani tani 65 za dhahabu kwa mwaka, huku wachimbaji wadogo wakichangia takribani asilimia 40 ya uzalishaji huo. Amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji hao kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na mnyororo wa thamani wa dhahabu.
Amesema hadi Juni 2026, viwanda vya ndani vilikuwa vimesafisha jumla ya kilogramu 36,776.37 za dhahabu ghafi, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa uwezo wa ndani wa kusafisha na kuongeza thamani ya dhahabu kabla ya kuingia katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za kifundi, utafiti na miundombinu ya maabara kwa ajili ya sekta ya madini. Mavunde amesema asilimia 10 ya mapato yatokanayo na sekta hiyo imetengwa kwa ajili ya utafiti, huku uwekezaji ukiendelea kufanyika katika maabara na miundombinu ya kisasa ili kuongeza usahihi wa taarifa za kijiolojia na upimaji wa madini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mh. Subira Mgalu ameitaka serikali kutupia jicho juu ya utitiri wa maabara za upimaji wa sampuli za madini ili kuhakikisha wadau wa sekta ya madini wanapata taarifa sahihi na zenye uhalisia.










