Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es salaam
Wamiliki na waendeshaji wa miundombinu muhimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini wametakiwa kujisajili ndani ya miezi sita kupitia mfumo maalumu wa CII Portal, ili kuwezesha miundombinu hiyo kupata ulinzi wa kisheria.
Usajili huo unatakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya mwaka 2015 na Tangazo la Serikali Na. 147, ambapo tangazo hilo lilitolewa Juni 19, 2026, hivyo kipindi hicho kinatarajiwa kumalizika Desemba 19, 2026.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 19, 2026, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo vya habari. Amesema Serikali imebainisha miundombinu muhimu ya TEHAMA kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ambayo inapaswa kusajiliwa na kulindwa.
Amesema miundombinu hiyo inahusisha mali, vifaa, mifumo ya kompyuta na mitandao inayoweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa usalama, uchumi na ustawi wa jamii, kiasi kwamba kutofanya kazi kwake kunaweza kusababisha athari kubwa nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, sekta zilizotajwa kuwa na miundombinu muhimu ya TEHAMA ni pamoja na Habari na Mawasiliano, Fedha na Benki, Maji, Afya, Nishati, Madini, Usafirishaji, Chakula na Kilimo, Ujenzi, Uchumi wa Buluu, Mazingira, Viwanda, Ulinzi, Anga, Elimu, Utawala wa Kiraia, Ulinzi wa Raia, Ardhi pamoja na Usalama na Utulivu wa Umma.
“Hatua hii inalenga kuhakikisha miundombinu yote inaendelea kuwa salama, inapatikana na kufanya kazi kwa uhakika hata wakati wa mashambulizi ya mtandao, hitilafu za kiufundi au majanga,” amesema Waziri.
Waziri Kairuki amesema Serikali pia imeandaa miongozo mitano kwa ajili ya kuwezesha wamiliki na waendeshaji kutambua na kusimamia miundombinu hiyo, ikiwa ni pamoja na Mwongozo wa Utambuzi na Usimamizi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA, Ukaguzi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA, Tathmini ya Hatari, Uadilifu na Uhalisia wa Data pamoja na Mipango ya Urejeshaji wa Huduma Baada ya Janga.
Amesema wamiliki au waendeshaji wa miundombinu hiyo wanapaswa kufungua akaunti kupitia CII Portal inayopatikana katika anuani ya cii.mawasiliano.go.tz kabla ya kuanza kuwasilisha taarifa za miundombinu yao.
Aidha, amewataka wadau wenye changamoto katika mchakato wa usajili au masuala ya kiusalama kushirikiana na wataalamu wa Wizara kupitia dawati la msaada.
Waziri Kairuki pia amesisitiza kuwa changamoto za kiusalama zinazohusisha miundombinu muhimu ya TEHAMA zinapaswa kuripotiwa kwa mamlaka husika ndani ya saa 24 tangu kubainika kwake.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amesema Serikali imeweka adhabu kali kwa mtu atakayebainika kuharibu miundombinu muhimu ya TEHAMA.
Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, mhusika anaweza kutozwa faini isiyopungua Sh milioni 100 au mara tatu ya hasara iliyosababishwa, au kifungo kisichopungua miaka mitano, au vyote kwa pamoja.
Aidha, taasisi, mashirika na wadau wote wanaomiliki au kuendesha miundombinu muhimu ya TEHAMA wameagizwa kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi na kwa wakati, huku wakizingatia matakwa ya sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.





