Na Happy Lazaro, Jamhuriedi, Arusha
AFRIKA imetakiwa kubadili mifumo na sera za ajira ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya kizazi kipya cha wafanyakazi, ikiwemo kuweka mazingira yatakayowezesha kazi za mbali na uchumi wa ajira za muda.
Wito huo umetolewa na Rais wa Zambia Institute of Human Resource Management ,Kelvin Shamizhinga, wakati akizungumza katika Mkutano wa Pili wa Maafisa Rasilimali watu barani Afrika unaojadili namna ya kubadilisha nguvu kazi ya Afrika kwa ajili ya mustakabali.
Shamizhinga amesema mkutano huo umewakutanisha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kwa lengo la kubadilishana uzoefu kuhusu mabadiliko yanayotokea katika usimamizi wa rasilimali watu na namna bara hilo linavyoweza kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Amesema moja ya maeneo muhimu yanayojadiliwa ni uchumi wa ajira za muda pamoja na kazi za mbali, akieleza kuwa maendeleo ya teknolojia yamefanya mtu kuwa na uwezo wa kufanya kazi kutoka eneo lolote bila kulazimika kuwepo katika ofisi ya mwajiri.
“Leo hii hatuwezi kukwepa ukweli kwamba wewe na mimi tunaweza kufanya kazi kutoka mahali popote. Kwa hiyo, ni muhimu kama bara kujadili aina ya mifumo, sera, taratibu na miongozo tunayopaswa kuweka ili kukidhi namna hii mpya ya kufanya kazi,” amesema.
Kwa mujibu wa Shamizhinga, waajiri wanapaswa kuandaa sera zitakazowezesha wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi wakiwa mbali na ofisi, bila hali hiyo kuathiri fursa zao za kupanda kiuchumi na kitaaluma ndani ya taasisi wanazofanyia kazi.
Amesema kuwa ,baadhi ya taaluma, ikiwamo ya watengeneza mifumo na programu za kompyuta (developers), hazihitaji mtu kuwa katika ofisi ya mwajiri ili kutekeleza majukumu yake, hivyo mashirika yanapaswa kuangalia zaidi matokeo ya kazi badala ya uwepo wa mfanyakazi ofisini.
Shamizhinga amesema mfumo wa kuhesabu kazi kwa kuangalia mfanyakazi ameingia kazini saa 2:00 asubuhi na kutoka saa 11:00 jioni pekee haupaswi kuendelea kuwa kipimo kikuu cha utendaji, akieleza kuwa mtu anaweza kuwepo ofisini kwa muda wote lakini akazalisha matokeo kidogo.
Amefafanua kuwa, badala yake, taasisi zinapaswa kuweka viashiria na viwango vya matokeo vinavyoweza kupimika, ili wafanyakazi waweze kuwajibika kwa kazi wanazozalisha na si kwa muda wanaotumia wakiwa katika eneo la kazi.
Ameongeza kuwa mfumo huo unaweza kusaidia taasisi kuongeza tija, kuwajumuisha watu wenye mitazamo na mazingira tofauti na pia kutoa nafasi kwa vizazi vipya kutumia maarifa, ujuzi na uwezo wao bila kulazimishwa kufuata mfumo mmoja wa kufanya kazi.
Shamizhinga amesema mabadiliko hayo yanahitaji nchi na taasisi za Afrika kushirikiana katika kuandaa sera na taratibu zitakazowezesha nguvu kazi ya bara hilo kuendana na teknolojia na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.
Mkutano huo umeandaliwa na Tanzania Human Resource and Administration Professionals Association (THRAPA) kwa kushirikiana na African Human Resources Confederation (AHRC) na umewakutanisha wataalamu na Maafisa Rasilimali Watu kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Mkutano huo wa siku nne unaofanyika kuanzia Agosti 19 hadi 22, 2026, unajadili namna ya kubadilisha na kuimarisha nguvu kazi ya Afrika ili iweze kukidhi mahitaji ya dunia ya sasa na siku zijazo.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu “Transforming Africa Workforce for the Future”, inayolenga kusukuma ajenda ya kujenga nguvu kazi yenye tija, ubunifu, ushindani na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia.


