23 Agosti 2026. | 📍Bagamoyo, Tanzania.
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) umeendelea kutoa mafunzo maalum ya siku mbili kuhusu Uongozi na Usimamizi wa Utekelezaji wa Mtaala Ulioboreshwa, yakilenga kuimarisha uwezo wa Wakuu wa Shule za Sekondari katika kusimamia kwa ufanisi mabadiliko ya mtaala.
Mafunzo hayo yameanza leo tarehe 24 na yatahitimishwa kesho tarehe 25 Agosti 2026 katika Kampasi ya ADEM Bagamoyo, yamewashirikisha Wakuu wa Shule za Sekondari 163 kutoka Mkoa wa Ruvuma na yamefadhiliwa na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA).
Katika mafunzo hayo, washiriki watajadili mada mbalimbali zinazolenga kuwajengea uwezo katika maeneo muhimu ya Uongozi na Usimamizi wa Shule, ikiwemo Uongozi na Usimamizi wa Shule, Usimamizi wa Utekelezaji wa Mtaala, Uchambuzi wa Mtaala Ulioboreshwa, Maadili na Itifaki pamoja na Huduma kwa Wateja.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Lucas Mzelela, amewapongeza washiriki kwa kutenga muda na kutumia rasilimali zao kushiriki katika mafunzo hayo, akieleza kuwa ni muhimu katika kuwawezesha viongozi wa shule kukabiliana kwa ufanisi na mabadiliko ya mtaala yaliyofanyika mwaka 2023.
Dkt. Mzelela amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa hiyo kwa kuzingatia kwa weledi mada zinazowasilishwa, kushiriki katika mijadala na kubadilishana uzoefu na wawezeshaji pamoja na washiriki wenzao.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa maadili katika utumishi wa umma, akieleza kuwa maadili na weledi vinapaswa kuzingatiwa katika mchakato mzima wa utoaji wa huduma za elimu, hususan kwa kuzingatia mahitaji ya wateja wa shule ambao ni wanafunzi, wazazi, jamii na wadau mbalimbali wa elimu.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuwawezesha Wakuu wa Shule kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, huku wakiongoza utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa kwa kuzingatia weledi, uwajibikaji na mahitaji halisi ya wanafunzi na jamii.
#ADEM #UongoziWaElimu #MtaalaUlioboreshwa #TAHOSSA #ElimuTanzania #SchoolLeadership #ADEMBagamoyo



