Na Mwandishi Wetu

Zaidi ya wanafunzi 95 wa Kitanzania wameondoka nchini kuelekea India kuanza masomo ya elimu ya juu katika vyuo mbalimbali, ikiwa ni kundi la kwanza kati ya wanafunzi 198 wanaotarajiwa kwenda kusoma nchini humo kupitia Global Education Link katika mwaka 2026.

Wanafunzi hao walioondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Terminal 3, jijini Dar es Salaam, wengi wao wamechagua programu zinazohusiana na sayansi, teknolojia na taaluma zinazohitajika katika dunia ya sasa, zikiwemo Computer Engineering, Cyber Security, Artificial Intelligence, Civil Engineering, programu mbalimbali za afya, sheria na biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Meneja wa Tawi la Dar es Salaam, Micky Musa, amesema kuondoka kwa wanafunzi hao ni sehemu ya mpango mpana wa kuwaunganisha vijana wa Tanzania na fursa za elimu ya kimataifa.

“Zaidi ya wanafunzi 95 wanaondoka katika kundi hili la kwanza kuelekea India, lakini kwa mwaka huu tunatarajia wanafunzi 198 kwenda kusoma nchini India. Hili si kundi la mwisho kwa sababu bado tuna wanafunzi wengine wanaoendelea kukamilisha taratibu zao,” amesema Musa.

Amesema mbali na India, Global Education Link inaendelea kuwaandaa wanafunzi wengine wapatao 185 wanaotarajiwa kuelekea nchini China, huku wengine wakiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi ya kwenda kusoma Malaysia, Marekani na Uingereza.

“Kadiri muda unavyokwenda Watanzania wataendelea kuona makundi mengine ya wanafunzi yakiondoka. Tunawaomba vijana wenye ndoto ya kusoma nje ya nchi wafike katika ofisi zetu zilizopo Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Arusha. Muda bado upo. Njoo na matokeo yako, nasi Global Education Link tupo tayari kukusaidia kuifanya ndoto yako kuwa uhalisia,” amesema.

Musa pia amewataka wazazi na walezi wenye vijana wanaotamani kupata elimu nje ya nchi kutumia ofisi za Global Education Link kupata ushauri kuhusu uchaguzi wa vyuo, programu za masomo, udahili, visa na maandalizi ya safari.

Miongoni mwa wanafunzi walioondoka ni vijana wanaokwenda kusomea Computer Science Engineering, Artificial Intelligence na Cyber Security, wakisema wamechagua taaluma hizo kutokana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na umuhimu wake katika maendeleo ya uchumi wa kisasa.

Alvin Andrew Munda, mwenye umri wa miaka 17, anayeelekea Lovely Professional University nchini India, amesema amechagua Computer Science kwa sababu anataka kujenga ujuzi wa vitendo katika teknolojia na baadaye kujikita zaidi katika Cyber Security.

Amesema mfumo wa masomo wenye nafasi kubwa ya mafunzo ya vitendo na matumizi ya maabara ulimvutia kuchagua chuo hicho.

“Napenda mfumo wenye practical zaidi kuliko kusoma theory na kuandika mitihani pekee. Nataka nitumie elimu nitakayoipata kutengeneza suluhisho na baadaye nijikite katika Cyber Security kwa sababu usalama wa mtandao ni muhimu sana katika dunia ya sasa,” amesema.

Akimshukuru Global Education Link, Munda amesema taasisi hiyo imeisaidia familia yake katika mchakato mzima, kuanzia kupata chuo hadi kukamilisha maandalizi ya safari.

“Global imenisaidia katika process nzima kabisa. Wametuelekeza hatua moja hadi nyingine na wamekuwa kiungo kati yetu, wazazi wetu na chuo mpaka tumefikia hapa airport tayari kuondoka,” amesema.

Mwanafunzi mwingine anayekwenda kusomea masomo yanayohusiana na Computer Science na Artificial Intelligence amesema anatarajia kuwa mtaalamu wa data na teknolojia katika miaka ijayo.

Amesema AI imeanza kuwa sehemu muhimu katika benki, hospitali, biashara, serikali na sekta nyingine, na hivyo anaamini elimu katika eneo hilo itamwezesha kuwa sehemu ya maendeleo ya kiteknolojia nchini Tanzania.

Naye mwanafunzi anayekwenda kusomea programu jumuishi ya Bachelor of Business Administration na Bachelor of Laws amesema ana ndoto ya kuwa mwanasheria na mfanyabiashara mwenye mafanikio baada ya kumaliza masomo yake.

Amesema Global Education Link imechangia kwa kiasi kikubwa kumfikisha katika hatua ya kuondoka kwenda masomoni.

“Global Education imetusaidia sana, hasa kwenye visa processing, kupata chuo na maandalizi mengine ya safari. Ushirikiano kati yangu, wazazi wangu na Global ndio umetufikisha hapa leo,” amesema.

Wazazi waliowasindikiza watoto wao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pia wameipongeza Global Education Link kwa namna ilivyosimamia mchakato wa watoto wao kuanzia hatua za awali hadi siku ya safari.

Donald Kito, mzazi wa Isaac Donald Kito anayekwenda Lovely Professional University kusomea Diploma ya Civil Engineering, amesema familia yake ilifahamu huduma za Global Education Link kupitia matangazo na baada ya kuwasiliana nao walipata maelezo yaliyowapa imani ya kuendelea na mchakato.