Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watu 11 kwa tuhuma za wizi, uharibifu na uhujumu wa miundombinu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).
Watuhumiwa hao, akiwemo Timoth Emesho maarufu kwa jina la Jack pamoja na wenzake 10, wanadaiwa kuhusika katika vitendo vya kuhujumu miundombinu ya mawasiliano ya shirika hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam Jumanne Muliro leo Agosti 27, 2026, watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kati ya miezi ya Juni, Julai na Agosti mwaka huu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa baadhi ya vitu vilivyokutwa kwa watuhumiwa hao ni nyaya za shaba zinazodaiwa kuwa mali ya TTCL pamoja na vifaa mbalimbali vinavyodaiwa kutumika kutekeleza uhalifu, ikiwemo sururu, kofia ngumu, reflector, misumeno na nguzo.
Jeshi la Polisi limelaani vitendo hivyo na kutoa onyo kali kwamba halitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kushiriki katika kupanga, kuiba, kusafirisha au kupokea mali zinazohusiana na miundombinu ya TTCL.
Aidha, Polisi imewapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa katika kuwafichua wahalifu na kuahidi kuendelea kulinda miundombinu ya taifa, watu na mali zao.


