Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Tanzania imefikia kiwango cha utoshelevu wa chakula cha asilimia 130, huku uzalishaji ukifikia tani 23.8 milioni katika mwaka wa fedha 2025/2026, huku Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ikisema hatua za kudhibiti visumbufu zimewezesha kuokoa zaidi ya tani milioni 1.4 za mazao ya nafaka.

Takwimu hizo zimetolewa leo Agosti 27, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Prof. Joseph C. Ndunguru, akieleza mafanikio ya Mamlaka kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na mipango ya mwaka 2026/2027.

Kwa mujibu wa Ndunguru, TPHPA imedhibiti kwelea kwelea milioni 233.5 katika wilaya 21, hatua iliyosaidia kuokoa takribani tani 1,092,780 za nafaka ambapo udhibiti wa viwavijeshi katika Halmashauri 52 uliwezesha kuokoa takribani tani 342,787.5 za mazao baada ya kutumika lita 54,846 za viuatilifu katika mashamba yenye ukubwa wa ekari 228,525.

Kwa upande wa masoko ya kimataifa, TPHPA imewezesha kampuni nane mpya za Tanzania kuanza kusafirisha parachichi kwenda China, na kufanya jumla ya kampuni zilizoruhusiwa kufikisha zao hilo katika soko hilo kufikia 24.

Pia, kampuni 444 za Tanzania zimesajiliwa katika mfumo wa forodha wa China (GACC) kwa ajili ya kusafirisha mazao mbalimbali.

Amesema Mamlaka hiyo pia imefungua masoko mapya kwa mazao ya Tanzania, yakiwemo parachichi kwenda Afrika Kusini, India na China, soya kwenda China, mashudu ya pamba na alizeti kwenda China, mahindi ya njano kwenda Misri, ndizi mbichi kwenda Afrika Kusini na mazao mbalimbali kwenda Seychelles.

” Hadi Juni 2026, soko la Seychelles lilikuwa limefunguliwa kwa mazao 10, yakiwemo kabichi, parachichi, maharage mabichi, karoti, viazi, tangawizi na nanasi,TPHPA imeendelea pia kulinda masoko yaliyopo,”ameeleza

Aidha amesemq Mamlaka ilichukua na kuchunguza sampuli 5,664 za mazao kwa kutumia teknolojia ya PCR ili kuthibitisha uwepo wa bakteria aina ya Xylella fastidiosa. Matokeo yalionesha Tanzania haina bakteria huyo, hivyo nchi ikaendelea kuruhusiwa kufanya biashara katika soko la Umoja wa Ulaya.

Katika udhibiti wa viuatilifu, amesema TPHPA ilikagua maduka 5,157, ikatoa vibali 3,831 vya kuingiza viuatilifu nchini na kusajili viuatilifu vipya 508. Pia sampuli 3,463 zilichukuliwa kwa uchunguzi, ambapo sampuli 132, sawa na asilimia nne, hazikukidhi viwango. Mamlaka iliondoa sokoni viuatilifu 205 vilivyobainika kuwa na viambata hatarishi na kufuta usajili wa viuatilifu 675 ambavyo havikuwa vimehuishwa kwa zaidi ya miaka 10.

Kwa upande wa teknolojia, TPHPA imenunua mashine tano za kisasa za maabara zenye thamani ya Sh2.8 bilioni, zikiwemo HPLC mbili, GC moja na GC-MS/MS mbili, zenye uwezo wa kuchakata zaidi ya sampuli 2,000 kwa wiki. Mamlaka pia imenunua magari 18, pikipiki 38, drones 21, vishikwambi 41 na Portable DNA Sequencers 19.

Katika mapato, TPHPA ilikusudia kukusanya Sh43 bilioni mwaka 2025/2026 na hadi Mei 2026 ilikuwa imekusanya Sh35.2 bilioni, sawa na asilimia 82 ya lengo, huku ikichangia Sh2.9 bilioni katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Mapato ya vituo vya mipakani nayo yalifikia Sh89.2 bilioni, kutoka Sh14.5 bilioni katika kipindi cha kulinganisha kabla ya maboresho.

Amefafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027, TPHPA imepanga kuongeza juhudi za kufungua masoko mapya, kulinda masoko yaliyopo, kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa mazao na kuongeza idadi ya kampuni zinazokidhi masharti ya masoko ya kimataifa. Mamlaka pia itaendelea na ujenzi na uboreshaji wa maabara katika vituo vya mipakani pamoja na maandalizi ya maabara mpya Tabora, Njombe na Mtwara.