Washington Dc,
Waziri wa Nishati na Makamu wa Rais Mteule, Mhe. Deogratius Ndejembi, amelipongeza Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa juhudi zake za kuwezesha uzinduzi wa Mpango wa Teknolojia za Atomiki Zilizopewa Leseni ya Matumizi ya Baharini (ATLAS), akieleza kuwa mpango huo ni hatua muhimu katika kuendeleza teknolojia bunifu za nyuklia na kuongeza matumizi ya nishati ya nyuklia duniani.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo wakati akizungumza katika Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Uzinduzi wa ATLAS unaofanyika tarehe 26–27 Agosti 2026 jijini Washington, D.C., Marekani.
Amesema mabadiliko makubwa yanayoendelea katika sekta ya nishati duniani yanazilazimu nchi kushirikiana katika kutafuta suluhisho zitakazowezesha kuimarisha usalama wa nishati, kukuza uchumi wa viwanda, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha wananchi wanapata nishati ya uhakika, nafuu na endelevu.
Akieleza hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kuimarisha upatikanaji wa nishati, Mhe. Ndejembi amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kutumia mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali vya nishati, ikiwemo umeme wa maji, gesi asilia, jua, upepo na vyanzo vingine vya nishati jadidifu.
Ameongeza kuwa Tanzania inaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya teknolojia bunifu za nishati, ikiwemo teknolojia za nyuklia, kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa nishati salama, ya uhakika na endelevu pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.









