TAKRIBAN watu 1,500 hawajulikani walipo nchini Nepal na katika eneo la Tibet nchini China, baada ya maporomoko ya barafu, miamba na udongo kusababisha mafuriko makubwa yaliyosomba makazi, barabara na madaraja katika eneo la Himalaya.

Polisi nchini Nepal walisema zaidi ya watu 165 wamefariki na wengine 826 hawajulikani walipo. Miongoni mwa waliopotea nchini humo, karibu 600 ni raia wa kigeni waliokuwa katika safari za utalii, kupanda milima au hija.

Nchini China, shirika la habari la serikali Xinhua limesema watu watatu wamefariki na wengine 558 hawajulikani walipo katika kaunti ya Gyirong, Tibet. Televisheni ya taifa CCTV imesema watu 260 kati ya waliopotea katika eneo hilo ni wageni.

Waokoaji nchini Nepal wanatumia helikopta kutafuta manusura na kusambaza chakula, mahema na vifaa vingine kwa maelfu ya watu waliokwama. Zaidi ya wanajeshi na polisi 5,000 wametumwa katika maeneo yaliyoathirika.

Video kutoka eneo la mpaka zinaonyesha maji yaliyochanganyika na matope na mawe yakisomba watu, magari na majengo. Manusura mmoja, Keshav Prasad Baral, amesema alijaribu kumshika mkono mkewe walipokuwa wakikimbilia juu ya nyumba, lakini mwanamke huyo alisombwa na matope.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa maporomoko ya barafu na miamba yaliingia katika Mto Lhende na kuachia mkondo mkubwa wa maji na vifusi. Shirika la Jiolojia la Marekani, USGS, limesema mtikisiko uliorekodiwa haukusababishwa na tetemeko la ardhi, bali nishati iliyotokana na maporomoko hayo.