Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema Zanzibar haitofikia maendeleo ya kweli pasi na kuwepo Baraza makini la Wawakilishi, linalosimamia maslahi ya Umma na matakwa ya Wananchi.
Amesema Zanzibar katu haitonyooka hadi kuwepo na Baraza madhubuti la Wawakilishi, linaloweza kuihoji Serikali na kuwawajibisha viongozi, hasa wabadhirifu, pale wanapokiuka misingi ya utawala bora.
Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza Mstaafu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ameyasema hayo leo Agosti 26 2026, huko Dunga Wilaya ya Kati Unguja, wakati akiwa katika Ziara yake ya Kuwaeleza Wananchi kuhusu Mustakbali wa Makubaliano na Maridhiano ya Kisiasa hapa Visiwani.
Amesema Baraza la Wawakilishi likiwa imara na likatekeleza ipasavyo Jukumu lake la Kuisimamia Serikali, litapelekea viongozi nao kuwa makini katika matumizi ya rasilimali za umma, na hatimaye utekelezaji wa majukumu yao.
“Viongozi watachelea kutenda ubadhirifu au ufisadi, pindipo wakihisi lipo Baraza litakalowahoji wakati wowote,” amesema Othman.
Ameongeza kuwa hata vitendo vya ufisadi vitapungua, pindipo Chombo cha Kutunga Sheria Nchini kitakuwa makini katika kuisimamia na kuihoji Serikali.
Aidha, Othman amefahamisha akisema iwapo Chama cha ACT Wazalendo kitashika Madaraka ya Kuiongoza Dola, anaamini wapo baadhi ya Wasaidizi wake makini, watakaoweza kutekeleza jukumu la kuinyoosha Nchi, sambamba na Baraza la Wawakilishi, ili kuhakikisha ufanikishaji wa maendeleo, na utekelezaji wa matarajio ya Wananchi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, alisema Chama hicho kinajivunia uwepo wa Safu imara ya Watendaji, chini ya Uongozi wa Mwenyekiti Othman Masoud Othman, hasa kutokana na dhamira yake ya kuijenga Zanzibar mpya, yenye utawala bora unaosimamia haki na maadili.
Naye, Mwenyekiti Mstaafu wa ACT Wazalendo, ‘Babu’ Juma Duni Haji, ametangulia kusema iwapo Makubaliano na Maridhiano ya Kisiasa yaliyofikiwa hivi karibuni yatatekelezwa kwa nia safi na yatapewa uzito unaostahiki, bila ya kinyongo, Wananchi wote bila ya kujali Itikadi za Kisiasa, watarajie mafanikio na manufaa makubwa.
‘Babu’ Duni amesema utekelezaji wa makubaliano hayo unaweza kuimarisha hali za maisha ya wananchi, pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, zikiwemo elimu na matibabu bora.
“Vurugu zimepitwa na wakati. Sasa tukaeni pamoja, hatutaki tena fujo, imetosha; twendeni tukatekeleze tuliyokubaliana kwaajili ya maslahi na manufaa ya Nchi yetu,” amesisitiza ‘Babu’ Duni.
Mapema, Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe, amewahimiza Wananchi wa Wilaya ya Kati kuunga-mkono Makubaliano yaliyofikiwa, kwa lengo la kuondoa mkwamo wa kisiasa hapa Visiwani.
Amesema wananchi wakiyasimamia na kuyaunga-mkono Makubaliano hayo, wale wasiopendelea maslahi ya Zanzibar wataondoka wenyewe madarakani.
Katika ziara hiyo, Othman aliambatana na Viongozi na Watendaji mbalimbali wa Chama hicho, akiwemo Katibu wa Habari na Uenezi Taifa, Salim Biman; Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kupitia ACT Wazalendo, Prof. Omar Fakih Hamad; Makamu Mwenyekiti wa Ngome ya Wazee, Masoud Khamis; na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini, Muhammed Khamis.












