Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Wakati vijana zaidi ya 23,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini wakisaka nafasi za kujiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), chuo hicho kimeeleza kuwa kina uwezo wa kudahili wanafunzi 7,500 pekee kwa mwaka wa masomo 2026/2027, hali inayoonyesha kwa kiasi kikubwa ongezeko la mahitaji ya elimu inayolenga kilimo, mifugo, mazingira, teknolojia na sekta nyingine shirikishi.

Kwa sasa SUA ina wanafunzi 17,438, idadi ambayo imeongezeka kutoka 15,479 mwaka 2022/2023, sambamba na uwekezaji mkubwa unaofanyika katika miundombinu na programu za kitaaluma.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Agosti 31, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Tihelwa Chibunda, amesema ongezeko hilo ni sehemu ya mabadiliko makubwa yanayoendelea chuoni hapo, yakichagizwa na mahitaji ya wataalamu katika uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mazingira ya kuongeza uwezo wa chuo katika kutoa elimu bora, kufanya utafiti na kuzalisha teknolojia zinazoweza kutumika katika kutatua changamoto za wananchi.

Kwa mujibu wa Prof. Chibunda, SUA sasa ina programu 58 za shahada za uzamili, Shahada za Awali 32, Stashahada za Juu mbili na programu sita za stashahada, huku wanafunzi 13,221, sawa na asilimia 86.5 ya wanafunzi wa shahada za kwanza, wakinufaika na mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.

Amesema Chuo hicho pia kimezalisha zaidi ya wahitimu 53,311 tangu mwaka 1985, wakiwemo wataalamu wanaoshiriki katika sekta mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.

Amesema mahitaji hayo makubwa ya elimu yamekwenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu, ambapo kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), SUA inatekeleza ujenzi wa majengo tisa ya kimkakati katika Kampasi za Morogoro na Mizengo Pinda mkoani Katavi.

Miradi hiyo inahusisha majengo makubwa ya taaluma yenye uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 3,000 kwa wakati mmoja, mabweni yenye uwezo wa zaidi ya wanafunzi 600 kila moja, jengo la TEHAMA na Uhandisi pamoja na maabara tatu za kisasa za kibayoteknolojia na tiba.

Prof.Chibunda amesema uwekezaji huo umefanya thamani ya mikataba ya ujenzi wa miradi ya HEET kufikia zaidi ya Sh56.3 bilioni, huku fedha zaidi ya Sh32 bilioni zikiwa tayari zimelipwa au kuthibitishwa na utekelezaji wa ujenzi ukiwa umefikia wastani wa asilimia 81.

” Kampasi ya Mizengo Pinda imefikia asilimia 93 ya utekelezaji wa miundombinu yake, huku Serikali ikiwa tayari ilitoa Sh1.7 bilioni kama fidia kwa wananchi 197 wa Kata ya Kibaoni, Mpimbwe, na kuwezesha chuo kupata ekari 689 kwa ajili ya upanuzi,”ameeleza

Katika utafiti, ameeleza kuwa SUA imeendelea kujenga nafasi yake kama kituo muhimu cha ubunifu na utatuzi wa changamoto za Taifa, ikiwa na miradi 172 ya utafiti inayoendelea kutekelezwa.

Amesema Tafiti hizo zimejikita katika kilimo, mifugo, afya ya wanyama na binadamu, mazingira, mabadiliko ya tabianchi, viumbe maji na maliasili. Chuo pia kimefanikiwa kupata hataza 16 za kimataifa, huku kikizalisha wastani wa machapisho 500 ya kitaalamu kila mwaka katika majarida yanayotambulika kitaifa na kimataifa.

Miongoni mwa tafiti zinazotajwa kuwa na matumizi ya moja kwa moja kwa jamii ni teknolojia ya panya buku wanaofundishwa kunusa vimelea vya kifua kikuu, mabomu na nyara za Serikali.

“SUA pia imefanya utafiti wa kutumia bundi kudhibiti panya waharibifu katika mashamba, huku ikiendelea na utafiti wa kutumia harufu bandia kuwazuia panya na wanyamapori kuingia katika maeneo ya uzalishaji,”amesema.

Kwa upande wa wataalamu,ameeleza wanataaluma 108 wako katika masomo ya shahada za umahiri na uzamivu, huku wengine 28 kutoka mataifa mbalimbali wakiwa wamepokelewa chuoni kama wasomi wa kimataifa.

Mbali na taaluma na utafiti, SUA imeanza kuimarisha uzalishaji na ujasiriamali ili kuongeza fursa kwa wanafunzi na mapato ya chuo. Kupitia SUA-STEP, vikundi 40 vya wanafunzi wajasiriamali vimesajiliwa na kupewa fursa za kufanya kazi ndogondogo za chuo, huku Kampuni ya SUA Income Generation & Services Ltd ikiandaliwa kusimamia shughuli mbalimbali za kibiashara.

Ametaja miongoni mwa maeneo hayo ni shamba la biashara, kiwanda cha samani, uchapishaji, uzalishaji wa chakula cha mifugo na shughuli za biashara katika Msitu wa Ifinga wenye hekta 10,000.

Prof. Chibunda amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, kipaumbele cha SUA ni kukamilisha miradi ya HEET, kuongeza uwezo wa maabara na vituo vya utafiti, kuimarisha shughuli za uzalishaji mapato na kuendeleza mafunzo yanayowajengea vijana ujuzi wa kujiajiri.

” Chuo pia kinalenga kuimarisha SUA Media, ikiwemo kufufua SUA TV na kuongeza masafa ya 101.1 SUA FM ili kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu ya kilimo, mifugo, uvuvi na mazingira,”amesisitiza.

Amesema mwelekeo huo unaifanya SUA isiwe taasisi ya kuzalisha wahitimu pekee, bali kuwa kitovu cha maarifa, utafiti, teknolojia na biashara kinacholenga kuongeza tija katika sekta zinazobeba uchumi wa Tanzania.