Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amekutana na Naibu Mufti na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa na Mkurugenzi wa Mufti Bima Foundation, Sheikh Ally Hamis Ngeruko na kujadiliana kuhusu mpango ya Mufti Bima Foundation wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kugharamia bima ya afya kwa kuwalipia huduma hiyo.
Majadiliano hayo yamefanyika Agosti 31 katika ofisi ndogo ya Prof. Shemdoe jijini Dar es Salaam, ambapo Sheikh Ngeruko ameeleza kuwa mpango huo ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo iliyo chini ya Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakary Zubeiry bin Ally katika kuunga mkono azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kupitia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Kwa upande wake, Prof. Shemdoe amepongeza uamuzi wa Mufti Mkuu na uongozi wa Mufti Bima Foundation kuanzisha mpango huo wenye lengo la kuwasaidia wananchi wenye uhitaji, hususan wale ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za bima ya afya, na kuongeza kuwa OWM – TAMISEMI ipo tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo pindi itakapohitajika.
Ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada hizo, Prof. Shemdoe amechangia kiasi cha Shilingi Milioni 1.5 ili zitumike kuwachangia wanufaika kumi wa Mufti Bima Foundation.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka viongozi wa Mufti Bima Foundation kushirikiana kwa karibu na taasisi binafsi na wadau mbalimbali katika Halmashauri ili kupata uwezeshaji na kuimarisha utekelezaji wa mpango huo.









