Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa wito kwa nchi wanachama wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) kuunganisha sauti na misimamo yao ili zisibaki kusikika pekee, bali ziwe na uzito na ushawishi katika maamuzi ya kimataifa, akisisitiza kuwa NAM inapaswa kuendelea kuwa sauti imara ya mataifa yanayoendelea katika kutetea usawa, amani, sheria za kimataifa na mfumo wa dunia wenye uwakilishi wa haki.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 01 Septemba 2026, jijini Belgrade, Jamhuri ya Serbia, alipowasilisha hotuba kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Kumbukumbu ya Miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa NAM.
Amesema misingi iliyoanzisha NAM mwaka 1961 bado ina umuhimu mkubwa katika mazingira ya sasa ya dunia, hususan wakati ambapo mataifa yanakabiliwa na changamoto za kisiasa, kiuchumi na kiusalama zinazohitaji ushirikiano, kuheshimiana na uhuru wa kila taifa kufanya maamuzi kwa maslahi yake.
Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa kutofungamana na upande wowote hakumaanishi kutokuwa na msimamo, bali ni uhuru wa mataifa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi yao, kulinda uhuru wa kisiasa na kujiamulia mustakabali wao bila kulazimishwa kujiunga na misimamo ya mataifa yenye nguvu.
Ameeleza kuwa kwa Tanzania, msimamo huo una mizizi katika falsafa na uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliona kutofungamana na upande wowote kuwa sehemu muhimu ya kulinda uhuru wa mataifa madogo na kuyawezesha kushiriki katika masuala ya kimataifa.
Katika kuimarisha amani duniani, Rais Dkt. Mwinyi amesema migogoro haiwezi kutatuliwa kwa kutumia nguvu, bali mataifa yanapaswa kuwekeza zaidi katika mazungumzo, upatanishi, kuzuia migogoro na kujenga kuaminiana, sambamba na kushughulikia vyanzo vya migogoro kwa kukosa haki, usawa na ujumuishi.
Aidha, ametoa wito wa kufanyika kwa mageuzi katika Mfumo wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo Baraza la Usalama, pamoja na taasisi za fedha za kimataifa, ili ziwe na uwakilishi mpana zaidi, uwazi na uwezo wa kuzingatia mahitaji ya mataifa yanayoendelea.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Afrika inapaswa kuwa na uwakilishi mkubwa na wa haki zaidi katika maamuzi ya kimataifa, kutokana na nafasi yake, idadi ya watu na rasilimali muhimu ilizonazo.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa Kusini, ikiwemo kuongeza uwezo wa Kituo cha Kusini cha Maarifa na Ushauri kwa Nchi Zinazoendelea (South Centre) katika kutoa tafiti, ushauri wa kitaalamu na kuimarisha nafasi ya nchi zinazoendelea katika majadiliano ya kimataifa.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameeleza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya NAM na BRICS, hususan katika maeneo ya fedha za maendeleo, ushirikiano wa Kusini na mageuzi ya mfumo wa utawala wa kimataifa, bila kuathiri uhuru, utambulisho na misingi ya NAM.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono NAM kuwa Harakati yenye umuhimu, umoja na malengo yanayoendana na changamoto za sasa, kwa kuhimiza amani, ushirikiano wa Kusini, haki ya maendeleo na mageuzi ya mfumo wa utawala wa dunia.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu “Urithi wa Kutofungamana na Upande Wowote: Mafunzo kwa Dunia ya Leo,”(The Legacy of Non-Alignment: Lessons for Today’s World) umefunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Aleksandar Vučić, na kuhudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Serikali pamoja na Wakuu wa Ujumbe kutoka mataifa 34.












