Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imeanza kujiandaa kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua za El Niño, ikitaja kumbukumbu za mafuriko, maporomoko ya ardhi, uharibifu wa miundombinu na milipuko ya magonjwa iliyowahi kutokea nchini katika misimu iliyopita kuwa sababu ya kuongeza tahadhari.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, hali hiyo imeifanya Serikali kuandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño, unaokadiriwa kuhitaji rasilimali za takribani Sh730 bilioni kwa ajili ya kutekeleza hatua mbalimbali kabla, wakati na baada ya maafa kutokea.

Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu na Wenye ulemavu Prof. Palamagamba Kabudi ameeleza hayo leo Sept 2,2026 Wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mpango wa taifa wa dharula wa kukabiliana na madhara ya El nino.

Amefafanua kuwa Sh730 bilioni si fedha zote zilizotengwa moja kwa moja katika bajeti ya Serikali kwa ajili ya El Niño, bali ni makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutoka Serikali, taasisi, sekta na wadau mbalimbali katika kutekeleza shughuli zilizoainishwa kwenye mpango huo.

Amesema makadirio ya Sh730 bilioni yamezingatia historia hiyo ya madhara, ukubwa wa utabiri wa msimu wa 2026/27 pamoja na uchambuzi wa athari zinazoweza kujitokeza katika sekta mbalimbali.

“Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27, kiasi cha Sh10 bilioni kimetengwa kwa ajili ya shughuli zinazohusiana na mpango huo katika sekta zote, Wizara, Taasisi na wadau wengine wanatakiwa kutumia bajeti zao kutekeleza maeneo yaliyoainishwa kulingana na vipaumbele vyao,”amesema

Amesema Mpango huo umeandaliwa baada ya Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) kutoa utabiri wa msimu wa Vuli Agosti 18, 2026, ukionyesha uwepo wa El Niño yenye nguvu, hali inayoweza kuongeza uwezekano wa mvua kubwa na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya mlipuko, uharibifu wa makazi na miundombinu pamoja na upotevu wa mali.

Amesema kwa serikali ,taarifa hiyo ni Kengele ya tahadhari ambayo imeungwa mkono na historia ya Tanzania, ambako misimu ya El Niño ya mwaka 1997/98, 2015/16 na 2023/24 ilihusishwa na madhara mbalimbali yaliyogusa maisha ya wananchi, shughuli za kiuchumi na miundombinu.

Kutokana na hali hiyo ameeleza kuwa Serikali imeweka mkazo katika kuzuia madhara kabla hayajatokea, badala ya kusubiri maafa yatokee ndipo hatua zichukuliwe.

Ametaja Miongoni mwa hatua zilizopangwa ni kufanya ukaguzi, ukarabati na uimarishaji wa miundombinu muhimu katika maeneo hatarishi, ikiwemo barabara, madaraja, makalavati, reli na mitaro, pamoja na miundombinu ya afya, elimu, usafiri, umeme, maji safi, maji taka na mawasiliano.

“Serikali pia imeagiza kuimarishwa kwa hifadhi ya akiba ya chakula na kuhakikisha vifaa vya uokoaji pamoja na misaada ya kibinadamu vinapatikana katika maghala ya kikanda ili viweze kutumika haraka endapo maafa yatatokea,”ameeleza

Aidha, amesema maeneo salama yanatakiwa kubainishwa na kutengwa mapema kwa ajili ya kuwa makazi ya muda kwa wananchi ambao wanaweza kulazimika kuhamishwa kutoka maeneo hatarishi kutokana na mafuriko au majanga mengine.

Tahadhari nyingine ni afya, ambapo Serikali imepanga kuandaa na kutekeleza mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea, huku usimamizi wa mazingira ukipewa kipaumbele.

Prof.Kabudi amesema hatua hizo zinahusisha udhibiti wa taka ngumu, usafishaji wa njia za maji, uimarishaji wa kingo za mito na mabwawa pamoja na kuhakikisha mitaro, makalavati na madaraja vinakuwa katika hali nzuri ili kuruhusu maji kupita bila kusababisha madhara makubwa.

Pamoja na maandalizi hayo,amewataka wananchi kutolichukulia tishio la El Niño kama chanzo cha hofu pekee, bali kutumia mvua hizo kama fursa ya kuongeza uzalishaji katika kilimo, ufugaji, uvuvi na uvunaji wa maji.

“Wananchi wanatakiwa kutumia mbinu bora za kilimo, kuchagua mazao na mbegu zinazofaa kwa msimu wa Vuli na kuhakikisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii zinafanyika katika maeneo salama,tumewaelekeza pia Wakuu wa Mikoa ambayo, kwa mujibu wa utabiri wa TMA, inaweza kuathiriwa na mvua za El Niño, kuchukua hatua za maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza,”amesema na kuongeza;

Taarifa sahihi ni sehemu ya uokoaji, hivyo wananchi wanatakiwa kufuatilia taarifa za TMA mara kwa mara na kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika pindi maafa yanapotokea,Vyombo vya habari na wadau wengine pia toeni taarifa sahihi kuhusu El Niño ili kuondoa taharuki isiyo ya lazima na badala yake kuwawezesha wananchi kuchukua hatua kwa wakati,”amesisitiza