Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Samia Kalamu Awards (SKA) Mhandisi Peter P. Mwasalyanda amesema jumla ya mawasilisho 294 yamefuzu kuingia hatua ya kupigiwa kura na wananchi katika Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo Samia Kalamu Awards 2026.
Mwasalyanda anasema hayo wakati akieleza hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya msimu wa pili wa tuzo hizo akisema kazi hizo zimefuzu baada ya kukamilika kwa zoezi la upokeaji na tathmini ya kazi zilizowasilishwa na washiriki.
Alisema jumla ya kazi 3,003 ziliwasilishwa na waombaji 985 na kufanyiwa tathmini na jopo la majaji kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa.
“Baada ya mchakato huo wa tathmini majaji waliteua mawasilisho 294 yaliyopata alama za juu na hivyo kufuzu kuingia katika hatua ya upigiwaji kura na wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa,kura za wananchi ni sehemu muhimu ya mchakato wa kumpata mshindi kwa kuwa zinawapa wananchi kama watumiaji wa maudhui ya habari na makala za maendeleo nafasi ya kutambua na kuunga mkono kazi wanazoona zimefanya vizuri na kuwa na mchango chanya kwa jamii.
Aidha ushiriki wa wananchi pia unatoa fursa kwa jamii kutoa mtazamo kuhusu thamani na umuhimu wa maudhui yanayozalishwa na waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini.
Mwasalyanda anasema zoezi la upigaji kura litaanza Septemba 3, 2026 na kukamilika Septemba 30, 2026, ambapo wananchi wataweza kushiriki kupitia tovuti rasmi ya tuzo hiyo au kwa kutumia ujumbe mfupi wa maandishi.
Alisema wananchi wanaweza kupiga kura kupitia tovuti ya www.samiaawards.tz, huku wale watakaotumia SMS wakitakiwa kutuma neno “SKA” likifuatiwa na namba ya mshiriki kwenda 15200.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kuunga mkono kazi za waandishi wa habari na vyombo vya habari ambazo kwa mtazamo wao zimekuwa na tija kwa jamii, ikiwamo kuibua na kuelimisha kuhusu masuala muhimu ya maendeleo.
Akizungumzia umuhimu wa tuzo hizo, Mwasalyanda alisema Samia Kalamu Awards inalenga kutambua kuenzi na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari na utayarishaji wa makala za maendeleo nchini.
Tuzo hizo zinaratibiwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB).


