Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kuimarisha miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Igunga kwa kutekeleza miradi mbalimbali yenye lengo la kuongeza upatikanaji na uhakika wa umeme katika maeneo ya Wilaya hiyo.

Mhe. Makamba amesema hayo leo, Septemba 3, 2026, katika Bunge la 13, Mkutano wa Nne, Kikao cha Saba, jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Manonga, Mhe. Abubakar Alli Omari, aliyeuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ziba, kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Amesema Serikali kupitia TANESCO tayari imekamilisha ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ya msongo wa Kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 41 kutoka Kituo cha Kupoza Umeme cha Lusu, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kudhibiti Mifumo ya Umeme (Switching Station) katika eneo la Ziba.

“Ujenzi wa Kituo cha Kudhibiti Mifumo ya Umeme (Switching Station) katika eneo la Ziba umekamilika na umeendelea kusaidia kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Igunga,” amesema Mhe. Makamba.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na hatua za kuimarisha zaidi miundombinu ya umeme katika Wilaya ya Igunga, ambapo TANESCO inatarajia kuanza kufanya Upembuzi Yakinifu wa Awali (Pre-Feasibility Study) kwa ajili ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Igunga.