Na Mwandishi wetu,Songea.

Wananchi Mkoani Ruvuma wameiomba serikali kupitia Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuona umuhimu wa kuchukua hatua za kuboresha miundombinu ya barabara ikiwa ni pamoja na kusafisha mifereji na mitaro ya kupitishia maji kabla ya wakati na baada ya mvua kubwa kunyesha na kipindi cha Elnino kinachotarajiwa kutokea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili walisema kuwa mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) ilisha toa tahadhali ya kuwepo kwa mvua kubwa na kuwepo kipindi cha Elnino jambo ambalo linahitaji serikali kuona umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara hasa maeneo korofi na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa wafanya biashara wa masoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nico Charles akizungumza na gazeti hili mjini Songea kuhusiana na tahadhari ya mamlaka ya hali ya hewa iliyotolewa kwa uma ameiomba serikali kupitia Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuona umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kusafisha mifereji inayopitisha maji ili mvua zitzkzpo anza kunyesha isiweze kuleta matatizo.

Mwenyekiti wa masoko Charles alifafanua Zaidi kuwa ni vyema kuangalia mapema maeneo yote ya madaraja pamoja na makalvati ambayo ni vivuko wakati wa masika au mvua zinapo endelea kunyesha ili yawe salama kwa kipindi chote ambapo alidai kuwa daraja la eneo la Mashale lililoko Mfaranyaki Manispaa ya Songea linanyufa kwa muda mrefu kutokana na mmomonyoko wa udongo uliopo kwenye bonde linaloelekea eneo la Majengo hivyo ni vyema kuona umuhimu wa kulifanyia matengenezo mapema hasa ikizingatia kuwa eneo hilo liko kwenye barabara ya kutoka Songea kuelekea Mbinga.

Njelela Haji Mkazi wa eneo la Mkuzo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea akizungumza na gazeti hili alisema kuwa hali ya miundombinu ya barabara ni mbovu sana hasa ya kutoka Mwenge Mshindo kupitia Mkuzo hadi Msamala ambayo wakati mvua zinavyo nyesha barabara hiyo huwa inajifunga hivyo ameiomba serikali iangalie uwezekano wa kuifanyia mategenezo brabara hiyo ambayo ni ya muhimu kabla mvua hazijaanza kunyesha hasa ikizingatiwa kuwa eneo la mwenge mshindo ni la Viwanda na Hospitali ya serikali ya Rufaa ilisha jengwa na imeshaanza kufanya kazi na wananchi wengi wanakwenda huko kupata huduma.

Felix Komba mkazi wa kijiji cha unyoni Wilaya ya Mbinga amesema kuwa hali za miundombinu ya barabara kwenye vijiji sio nzuri hivyo amesema kuwa iko haja ya serikali kuchukua hatua za haraka za kufanyia matengenezo kabla ya kipindi cha mvua na elnino jambo ambalo linaweza kusababisha kero kubwa ya wananchi wanapotaka kusafiri kutoka majumbani mwao kwenda kupata huduma Mbinga mjini au hospitali pale wanapo umwa.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Salehe Juma akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuhusiana na hali ya tahadhali ya mamlaka ya hali ya hewa alisema kuwa tayari ofisi yake imesha jipanga kwa kuhakikisha kuwa barabara zote zinazo unganisha Wilaya hadi Wilaya zinafanyiwa ukarabati na si vinginevyo.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Silvesta Chinengo alisema kuwa Tarura Mkoa wa Ruvuma inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kujiweka tayari kukabiliana na athali zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za elnino huku wakisimamia utekelezaji miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara pamoja na madaraja Mkoani humo.

Mhandisi Chinengo alisema hali ya mtandao wa barabara Mkoani Ruvuma ni mzuri hivyo wakala wa barabara vijijini na mijini Mkoani humo unahudumia jumla ya urefu wa kilomita 7,147,198 za mtandao wa barabara ambazo zimegawanyika katika makundi ya barabara za mkusanyo(collector Roads) kilomita 3,874,851,barabara za mjjazio(feeder Roads) zenye urefu wa kilomita 2,312,829 na barabara za jamii kijiji (community roads) zenye urefu wa kilomita 959,519.

Aisema kuwa aina ya barabara za kiwango cha lami ni kilomita 133,697, barabara za changarawe ni kilomita 1,651,867 na barabara za udongo ni kilomita 5,360,624 hivyo barabara hizo hupitika kwa kipindi cha mwaka mzima ingawa kunabaadhi ya maeneo yanakuwa na changamoto hasa katika kipindi cha masika hivyo serikali kupitia wakala wa barabara vijijini na mijini Mkoani humo inaendelea na mpango mkakati wa kuongeza kiwango cha barabara zinazopitika majira yote ya mwaka mzima.

Aidha Muhandisi Chinengo alisema kuwa mamlaka ya hali ya hewa imetoa taarifa kuhusu mwenendo wa mvua na hali ya hewa hivyo wakala wa barabara vijijini na mijini mkoani Ruvuma ni wadau wa mamlaka wa hali ya hewa Tanzania(TMA) na kwakawaidi wanatumia taarifa hizo kwa uzito mkubwa kwa sababu hali ya hewa inauhusiano wa moja kwa moja na usalama wa miundombinu ya barabara hivyo taarifa hizo zinawasaidia kufanya maandalizi ya mapema kutambua maeneo hatarishi,kupanga ukaguzi na matengenezo ya miundombinu pamoja na kutoa elemu kwa wananchi na kutoa tarifa ya usalama wa barabara wakati mvua zinapo nyesha na amesisitiza mapema kufanya maadalizi kwani kinga na bora kuliko kusubiri madhala yatokee.