Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema itaendelea kugharamia ada kwa wanafunzi wenye ulemavu wanaojiunga na vyuo vyake nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kundi hilo linapata fursa sawa ya kupata ujuzi na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema mwaka uliopita wanafunzi 145 wenye ulemavu waliodahiliwa katika vyuo vya mamlaka hiyo waligharamiwa ada, huku akiwahimiza watu wenye ulemavu kujitokeza kuomba mafunzo ya ufundi stadi kwa kuwa gharama zao za masomo zitalipwa kwa kipindi chote cha mafunzo.

Kasore ameyasema hayo leo Septemba 4, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu nafasi ya VETA katika kujenga taifa lenye wananchi wenye ujuzi na mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa VETA kuhakikisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanapatikana kwa watu wote bila kujali changamoto wanazokabiliana nazo, huku kundi la watu wenye ulemavu likipewa nafasi katika mipango ya kuongeza udahili na upatikanaji wa mafunzo.

Kwa mujibu wa Kasore, katika kipindi cha mwaka 2022/2023 hadi 2025/2026, jumla ya wanafunzi 88 wenye ulemavu walidahiliwa katika vyuo vya VETA, sambamba na wanafunzi 1,606 kutoka mazingira hatarishi na wanafunzi wa kike 32,421.

“Tunatambua kuwa elimu na mafunzo ya ufundi stadi yanapaswa kupatikana kwa watu wote, bila kujali jinsia, mahali wanapotoka au changamoto wanazokabiliana nazo,” amesema.

Amesema katika kipindi kijacho VETA itaendelea kuongeza ushiriki wa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wananchi wanaotoka katika mazingira magumu, kwa kutumia vyuo vipya, kozi fupi na mifumo nyumbufu ya utoaji mafunzo.

Hatua hiyo inaenda sambamba na mpango wa Serikali wa kukamilisha ujenzi wa vyuo vipya 65 vya VETA, ambavyo vinatarajiwa kuanza kutoa mafunzo Januari 2027, hatua itakayopanua zaidi fursa za wananchi kupata elimu na mafunzo ya ufundi stadi karibu na maeneo yao.

Kasore amesema vyuo hivyo vinatarajiwa kuongeza uwezo wa VETA kudahili wanafunzi wapya 130,892 mwaka 2027, huku msisitizo ukiwa si kuongeza idadi ya wanafunzi pekee, bali kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kuwawezesha kujiajiri.

Amesema VETA pia inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuongeza ujuzi, ikiwemo INTEP, SEP na RPL, huku ikipanua mafunzo katika sekta zenye mahitaji makubwa ya nguvu kazi kama kilimo, ujenzi, madini, nishati, TEHAMA, usafirishaji na uzalishaji viwandani.

Katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Kasore amesema VETA inalenga kuhakikisha mafunzo yanawafikia wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na watu wanaoishi katika mazingira magumu, kwa kutambua kuwa rasilimali watu yenye ujuzi ni msingi wa uchumi jumuishi na shindani.

Amesema kupitia juhudi hizo, VETA inalenga kujenga mazingira ambayo wananchi, wakiwemo wenye ulemavu, hawatalazimika kusubiri ajira pekee, bali watakuwa na ujuzi wa kujiajiri, kuajiri wengine na kuongeza thamani katika uchumi wa Taifa.