Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wananchi wananufaika na Biashara ya Kaboni kupitia misitu ikiwemo mikoko wanayopanda katika maeneo ya pwani.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Septemba 04, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kiwani Mhe. Hija Hassan Hija aliyetaka kujua kwa namna gani wananchi hasa wa visiwani wanafaidika na mfumo wa kupata mitaji na elimu ya biashara ya kaboni.

Akijibu swali hilo, alisema Serikali imeendelea kujenga uwezo kwa jamii kupitia mafunzo na huduma za ushauri, kuunganisha miradi ya biashara ya kaboni na masoko ya kimataifa hatua iliyochangia miradi 117 kusajiliwa.

Ili kuendelea kuleta manufaa kwa upande wa Zanzibar, Mhe. Kwagilwa alimuelekeza Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kushirikiana na Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika kuwajengea uwezo wananchi wa ili wafaidike na biashara ya kaboni.

Aidha, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa pamoja na kuwa suala la mazingira linalojumuisha NCMC si la Muungano, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ina inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza hifadhi ya mazingira.

“Kwenye eneo hili tuna maelekezo mahsusi kutoka kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyotoa alipofanya kikao na Wizara yetu alituelekeza kuhakikisha tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wanuifaike kwa kuhakikisha tunasajili miradi tunatoa huduma za kiushauri kwenye eneo la biashara ya kaboni, alisema Mhe. Kwagilwa.

Akijibu swali la Mbunge huyo kuhusu Serikali imeweka mikakati gani ya kuwawezesha wananchi kuongeza wigo wa kufanya biashara ya kaboni, Mhe. Kwagilwa alisema NCMC imeendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani kwa kuandaa mikakati na miongozo ya upatikanaji wa fedha ili kuvutia wawekezaji wa ndani katika miradi ya kaboni.

Halikadhalika, Naibu Kwagilwa alitaja mikakati mingine kuwa ni kuweka mifumo ya uwazi ya mgawanyo wa faida (benefit-sharing) na mikataba ya haki kwa jamii zinazohifadhi misitu na ardhi.

Tanzania ina fursa ya kunufaika na biashara ya kaboni kupitia rasilimali na mifumo ya kipekee ya bahari, maziwa, mito, ardhi na misitu yenye ukubwa wa hekta milioni 48.1 pamoja na ukanda wa eneo la mwambao wa bahari takriban kilomita 1,424 yenye mfumo muhimu wa bahari, mikoko na matumbawe.