Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeikabidhi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) tani 52 za dawa na vifaa tiba zenye thamani ya shilingi milioni 220, sawa na takribani dola 88,000 za Kimarekani, kusaidia mapambano dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Msaada huo umekabidhiwa leo, Septemba 5, 2026 jijini Kinshasa na Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence George Samizi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bidhaa zilizotolewa, zinajumuisha dawa, vifaa kinga kwa ajili ya wahudumu wa afya, vifaa tiba na mahitaji mengine kwa ajili ya kuimarisha huduma kwa wagonjwa na kukatiza mnyororo wa maambukizi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Samizi amesema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Tanzania katika majukwaa mbalimbali ya afya ikiwemo Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola uliofanyika kwa njia ya mtandao 16 Juni, 2026, katika kukabiliana na majanga ya kiafya ambayo hayatambui mipaka.
Kwa upande wake, Katibu wa Waziri wa Afya wa DRC, Dkt. Romain Muboyayi, ameishukuru Tanzania kwa msaada huo, akisema umeonesha undugu, urafiki na ushirikiano imara uliopo kati ya nchi hizo mbili chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.
Dkt. Muboyayi amesema vifaa hivyo vitaunga mkono juhudi za Serikali ya DRC za kudhibiti mlipuko wa Ebola na kuwalinda wahudumu wa afya wanaohudumia walioathirika.
Dkt. Samizi amesisitiza kuwa DRC itaendelea kushirikiana na Tanzania na washirika wa kikanda na kimataifa kuimarisha utayari, ufuatiliaji na mwitikio wa haraka dhidi ya milipuko na dharura za kiafya barani Afrika.












