Na Benny Mwaipaja, Kigali, Rwanda

Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa kuimarisha mifumo ya kuthibiti utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa silaha za maangamizi.

Mheshimiwa Balozi Omar amesema hayo jijini Kigali nchini Rwanda, wakati wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kupambana na Utakasishaji Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Silaha za Maangamizi (ESAAMLG), uliofanyika katika Hoteli ya Serena, nchini humo.

Alieleza kuwa nchi imefanikiwa katika tathmini ya pamoja (mutual evaluation) iliyofanywa na ESAAMLG kupitia Kamati ya Wataalam (Makatibu Wakuu) na kwamba Serikali inaendelea kufanyia kazi baadhi ya mapungufu yaliyoainishwa ili kuimarisha zaidi sekta ya fedha na maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii kwa ujumla.

“Tuna sheria na kamati ya kitaifa ya kupambana na masuala haya. Mafanikio ni makubwa, lakini bado kuna maeneo 15 tunayafanyia kazi, ikiwemo marekebisho ya sheria 12 zilizobainishwa kuwa zinahitaji maboresho kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Mhe. Balozi Omar alisema kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, sheria nne tayari zimepitishwa na Bunge katika kikao kinachoendelea, huku Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitarajiwa kuwasilisha muswada wa kurekebisha sheria nyingine tatu ili kukamilisha mchakato huo.

Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yalikuwa ni matokeo ya ushirikiano wa taasisi mbalimbali nchini, ikiwemo Wizara ya Fedha, wasimamizi wa sekta ya mabenki, Wizara ya Sheria, pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani na taasisi nyingine kadhaa zinazoshirikiana katika Kamati ya Kitaifa ya kupambana na vitendo hivyo.

Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa Serikali katika ngazi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Fedha, Katiba na Sheria, Mambo ya Ndani na maafisa waandamizi kutoka nchi wanachama wa Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika lengo likiwa kuimarisha juhudi za pamoja za kupambana na utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi, na ufadhili wa silaha za maangamizi.

Viongozi wengine kutoka Tanzania walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi na Kamishna wa Kitengo cha FIU, Bw. Majaba Magana

Wengine ni Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mwenyeti wa Kamati ya Kitaifa ya Wataalamu ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Haramu, Bi. Sauda Msemo, wakuu wa taasisi, wataalamu wa sekta ya fedha, wasimamizi wa taasisi za kifedha na wadau wengine wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali za ukanda huo na dunia kwa ujumla.