CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mwaka wa 2026 wa Alliance for African Partnership (AAP), utakaowakutanisha viongozi wa vyuo vikuu, wanazuoni, watunga sera, wabunifu, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kutoka Afrika na sehemu mbalimbali duniani.
Mkutano huo utafanyika Septemba 16 hadi 22, 2026, kwa ushirikiano kati ya UDSM na Michigan State University (MSU) ya Marekani, ukiwa na kaulimbiu “Kufikiria Upya Mustakabali wa Elimu ya Juu Barani Afrika: Uongozi, Ubunifu na Ushirikiano wa Kimataifa.”
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo–Utafiti wa UDSM, Profesa Nelson Boniface, amesema mkutano huo utajadili namna vyuo vikuu vya Afrika vinavyoweza kuimarisha uongozi katika utumishi wa umma, kuwaandaa wahitimu kukabiliana na mabadiliko ya soko la ajira, pamoja na kuendeleza utafiti, ubunifu na ushirikiano wenye manufaa kwa jamii.
Amesema mkutano huo utawakutanisha viongozi na wanazuoni mbalimbali, akiwamo Mkuu wa Taaluma wa MSU, Profesa Laura Lee McIntyre; Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere, Profesa Barnabas Nawangwe; Makamu Mkuu wa Lilongwe University of Agriculture and Natural Resources, Profesa Emmanuel Kaunda; Profesa Paul Zeleza, Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya AAP na Mkuu wa Ndaki ya Elimu ya MSU, Profesa Jerlando Jackson.
Kwa mujibu wa Profesa Boniface, Septemba 17 kutakuwa na Mdahalo wa Umma wa AAP–Andrew Carnegie Foundation kuhusu “Akili Unde na Mustakabali wa Ajira,” utakaofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah, UDSM.
Amesema Septemba 18 kutakuwa na kikao rasmi cha ufunguzi kitakachojumuisha mjadala wa ngazi ya juu kuhusu “Uongozi katika Utumishi wa Umma na Matokeo ya Kimataifa: Nafasi ya Elimu ya Juu,” pamoja na Jukwaa la Ubunifu litakalowakutanisha vyuo vikuu, wajasiriamali, wawekezaji na viongozi wa sekta za uzalishaji.
Shughuli nyingine zitakazofanyika ni maonesho ya utafiti, mijadala kuhusu mafanikio ya taasisi wanachama wa AAP na warsha zitakazojadili ufundishaji wa wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu, jinsia na ujumuishaji pamoja na usimamizi wa utafiti.
Profesa Boniface amesema mkutano huo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi, kuchochea ushirikiano mpya katika utafiti na ubunifu na kuimarisha dhamira ya AAP ya kuendeleza elimu ya juu inayoongozwa na Waafrika, sambamba na ushirikiano wa kimataifa wenye usawa.
AAP ni muungano unaoongozwa na vyuo vikuu, wenye kitovu chake Michigan State University, unaounganisha taasisi 12 kutoka nchi 10 za Afrika ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Malawi, Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe, Mali, Senegal na Nigeria.
UDSM, iliyoanzishwa mwaka 1961, imepewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na uzoefu wake katika elimu ya juu, utafiti na ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.



