Na Mwandishi wetu–Jamhuri Media
Dar es salaam
Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Priscus Kiwango, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kidijitali na utoaji wa huduma za umma kwa njia ya kielektroniki kupitia Mradi wa Digital Tanzania (DTP), unaotarajiwa kukamilika rasmi Oktoba 31, 2026.
Amesema hayo leo, Septemba 14, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mkutano wa Wadau wa Mradi wa Digital Tanzania, unaofanyika kwa siku tatu kwa lengo la kubainisha mafanikio ya mradi huo katika sekta ya mawasiliano ya kidijitali.
“Mradi huu umewezesha kujengwa na kuboreshwa kwa miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo minara katika maeneo ya vijijini ambayo yalikuwa na changamoto ya mawasiliano, kwani hayakuwa na huduma ya uhakika ya mawasiliano,” amesema Kiwango.
Hata hivyo, amesema tangu mradi huo uanze mwaka 2021, umefadhiliwa kwa mkopo wa Dola za Marekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia, ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa intaneti na kuboresha utoaji wa huduma za Serikali kwa kutumia teknolojia.
Amesema wananchi katika maeneo hayo sasa wanaweza kupata huduma za mawasiliano kupitia mitandao ya 3G na 4G, huku taasisi za Serikali hadi ngazi ya Serikali za Mitaa zikiunganishwa katika mifumo mbalimbali ya kidijitali.
Miongoni mwa mifumo iliyowezeshwa kupitia mradi huo ni PEPMIS, unaotumika kupima utendaji wa watumishi wa umma, pamoja na Mfumo wa Daktari wa Huduma za Serikali, unaomwezesha mwananchi kupata taarifa kuhusu huduma zinazotolewa, muda wa kuzipata na gharama zake.
Naye Mratibu wa Mradi wa Digital Tanzania, Bakari Mwamgugu, amebainisha kuwa mradi huo unatekelezwa katika maeneo makuu matatu ambayo ni Ekolojia ya Kidijitali inayohusisha sheria, miongozo na sera za TEHAMA; Uunganishaji wa Kidijitali; pamoja na kuwajengea uwezo watumishi.
Pia amesema kupitia mradi huo, minara mipya 758 imejengwa, huku minara 304 ikiboreshwa kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema Serikali imeongeza uwezo wa intaneti kwa Gbps 60, ambapo Gbps 40 ni kwa Tanzania Bara na Gbps 20 kwa Zanzibar, hatua inayosaidia kupunguza gharama za matumizi ya intaneti kwa taasisi za umma.
Mradi huo pia umewezesha kuanzishwa kwa vituo 32 vya huduma pamoja (One-Stop Service Centers) katika majengo ya Posta, vinavyomwezesha mwananchi kupata huduma za NIDA, RITA, Jeshi la Polisi na Land Registry katika eneo moja.
Halikadhalika, amesema watumishi wa umma wapatao 500 wamepatiwa mafunzo kuhusu teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI), huku watumishi 50 wakipelekwa kusoma nje ya nchi katika ngazi ya uzamili, ikiwemo India, Singapore, China, Estonia, Finland na Malaysia.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Miundombinu, Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Issa Bakari, ameeleza kuwa mradi huo umewezesha kuanzishwa kwa Zanzibar Digital Services Directory (ZGSD), ZanPortal na vituo viwili vya One-Stop Center vilivyojengwa Posta Kijangwani, Unguja, na Chakechake, Pemba.
Bakari amesema zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Zanzibar sasa wanafikiwa na huduma za mawasiliano kuanzia 2G hadi 5G kupitia minara 63 iliyojengwa katika utekelezaji wa mradi huo.
“Kutokana na mafanikio yaliyopatikana, Serikali imeanza mazungumzo na Wizara ya Fedha pamoja na Benki ya Dunia kuhusu uwezekano wa kuingia katika awamu ya pili ya Mradi wa Digital Tanzania, itakayolenga kukamilisha na kuendeleza maeneo ambayo hayajakamilishwa katika awamu ya kwanza,” amesema Bakari.




