Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora
Muasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF), Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amehitimisha ziara yake ya siku nne mkoani Tabora kwa kutembelea na kukagua zahanati pamoja na nyumba mbili za watumishi zilizojengwa katika Kijiji cha Gengesita, Kata ya Kizengi, Wilaya ya Uyui.
Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Mradi wa Jamii Salama unaotekelezwa na JMKF kupitia huduma za kliniki tembezi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya afya katika maeneo ya pembezoni.
Akizungumza na vyombo mbalimbali baada ya ziara hiyo, Dkt. Kikwete alisema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa zahanati mbili ambazo sasa zimeanza kutoa huduma kwa wananchi. Aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano wake na JMKF katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Dkt. Kikwete pia aliishukuru kampuni ya Marekani ya S.C. Johnson & Son, ambayo ndiyo imefadhili miradi hiyo, kwa mchango wake katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wa maeneo ya pembezoni. Aidha, alizishukuru serikali za Mkoa wa Tabora pamoja na Wilaya za Uyui na Sikonge kwa ushirikiano waliouonesha tangu kuanza kwa utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa mujibu wa JMKF, kila zahanati imejengwa kwa lengo la kutoa huduma kamili za afya ya msingi, ikiwemo idara ya wagonjwa wa nje, kliniki ya afya ya uzazi na mtoto, wodi ya wazazi, vyoo vya umma, kichomea taka, mashimo maalumu kwa ajili ya kondo la nyuma pamoja na nyumba mbili za watumishi.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma za afya zinapatikana karibu na wananchi, huku makazi ya watumishi yakitarajiwa kusaidia upatikanaji na ubaki wa wataalamu wa afya katika maeneo ya pembezoni, hususan wauguzi wakunga.
Kwa miaka mingi, umbali umekuwa kikwazo kikubwa kwa wakazi wa vijiji vya Gengesita, kilicho takribani kilomita 152 kutoka ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, na Ipembe, kilicho takribani kilomita 199 kutoka ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge. Hali hiyo imekuwa changamoto zaidi kwa wajawazito, watoto, wazee na wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka.
Ujenzi wa zahanati hizo unatokana na mafanikio ya Mradi wa Jamii Salama ambao JMKF iliuendesha mwanzoni mwa mwaka 2025 kupitia kliniki tembezi, ambapo mamia ya kina mama wajawazito walipatiwa huduma muhimu za afya bila malipo.
Baada ya kuona ukubwa wa mahitaji ya huduma za afya katika maeneo hayo, JMKF iliamua kujenga zahanati hizo ili kuweka msingi wa huduma za kudumu kwa jamii zilizo mbali na vituo vya afya vya wilaya na mkoa.
JMKF inaendelea kushirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, hususan kwa jamii zilizo katika maeneo yenye changamoto ya umbali wa kufikia vituo vya kutolea huduma.











