Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma
Wakala wa Vipimo (WMA) imehakiki vipimo 1,166,995 nchini katika mwaka wa fedha 2025/2026, sawa na asilimia 92 ya lengo la vipimo 1,269,957, huku ikifanya kaguzi 5,015 katika maeneo mbalimbali ya biashara.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, ametoa takwimu hizo jijini Dodoma Septemba 9, 2026, wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30, 2026.
Kihulla amesema hatua hiyo ni sehemu ya jukumu la Wakala kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi vinakuwa sahihi, hatua inayolenga kulinda maslahi ya walaji, wafanyabiashara na wazalishaji.
Amesema vipimo vinavyohakikiwa vinahusisha maeneo mbalimbali yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, ikiwemo mita za maji, pampu za mafuta, mizani, malori ya kubeba mchanga, kokoto na vifusi pamoja na mitambo ya kupimia mafuta na vimiminika.
Kwa mujibu wa Kihulla, katika kipindi hicho WMA ilihakiki mita za maji 314,423, mizani midogo na ya kati 497,807, pampu za kuuzia mafuta 17,289 na mizani mikubwa (weighbridges) 1,725.
Aidha, Wakala ilihakiki malori 27,282 yanayobeba mchanga, kokoto na vifusi, tenki za magari yabebayo vimiminika 16,252, tenki za kuhifadhia mafuta ya nishati 7,381 na flowmeters 2,125 zinazotumika kupima vimiminika kwa mtiririko.
Kihulla amesema pamoja na uhakiki wa vipimo, WMA ilifanya kaguzi za kawaida na za kushtukiza katika maeneo mbalimbali ya biashara, ikiwemo maduka ya nyama, masoko, vituo vya kununulia mazao na maduka ya vifaa vya ujenzi.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wakala ilikuwa imepanga kufanya kaguzi 4,000, lakini ilifanikiwa kufanya kaguzi 5,015, sawa na asilimia 125 ya lengo.
Kulingana na maelezo yake, kaguzi hizo zililenga kuhakikisha mizani na vifaa vingine vya kupimia vinatumika kwa usahihi na kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Vipimo.
Kwa mwananchi anayenunua bidhaa kwa kilo, lita au kipimo kingine, usahihi wa kifaa kinachotumika kupimia ni muhimu katika kuhakikisha kiasi anacholipia ndicho anachopokea.
Kuhusu sekta ya kilimo, Kihulla amesema WMA imeendelea kukagua mizani inayotumika kupimia mazao ya kimkakati, yakiwemo korosho, pamba, kahawa na ufuta.
Amesema ukaguzi huo umefanyika katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi, Kigoma, Katavi na Kanda ya Ziwa.
Kwa msimu wa 2025/2026, amesema Wakala imeanza kuwezesha matumizi ya mizani janja (anti-tampering scales), inayomsaidia mkulima kupata taarifa ya kiasi cha mazao aliyouza mara baada ya kupima.
“Mizani hii pia inaiwezesha Wakala kupata taarifa endapo mzani utachezewa kinyume na taratibu,” amesema Kihulla.
Amesema matumizi ya mfumo huo yanaongeza uwazi katika upimaji wa mazao na kusaidia kuhakikisha mkulima analipwa kwa kuzingatia kiasi halisi cha mazao aliyoyauza.
WMA pia imeendelea kukagua bidhaa zilizofungashwa zinazozalishwa nchini na zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
Kihulla amesema katika kipindi cha mwaka mmoja kilichoishia Juni 30, 2026, jumla ya bidhaa 21,262 zilizozalishwa nchini zilikaguliwa, huku shehena 17,774 za bidhaa kutoka nje ya nchi nazo zikifanyiwa ukaguzi.
Amesema bidhaa hizo zilihusisha vifaa vya ujenzi kama vigae (tiles), saruji, nondo na mabati, pamoja na vinywaji na vyakula.
Kwa mujibu wa Kihulla, ukaguzi huo unalenga kuhakikisha bidhaa zinawafikia watumiaji kwa kiasi kilichoainishwa na mzalishaji.
Katika utekelezaji wa Mpango wa Kuhamasisha Matumizi ya Nishati ya Gesi Asilia, Kihulla amesema WMA inaendelea kuhakiki mita na vipimo vinavyotumika katika mnyororo wa gesi, kuanzia inapochakatwa hadi inapomfikia mtumiaji wa mwisho.
Amesema uhakiki huo unahusisha vituo maalumu vya kuuzia gesi vilivyopo Tazara, Ubungo, Dangote Mkuranga na Mtwara, Taqwa Airport, Mlimani City, TPDC Mlimani City na Mandela Road.
Pia, WMA inahakiki uzito wa mitungi ya gesi inayofungwa kwenye vyombo vya usafiri ili kujiridhisha na usahihi wa vipimo vyake.
Wakala wa Vipimo ina historia inayorejea mwaka 1884, wakati shughuli za uhakiki na ukaguzi wa vipimo zilipoanza chini ya utawala wa Kijerumani.
Baada ya Uhuru, Idara ya Vipimo iliendelea kufanya kazi chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara hadi Mei 17, 2002, ilipopandishwa hadhi na kuanzishwa rasmi kuwa Wakala wa Vipimo.
Mabadiliko hayo yalilenga kuongeza ufanisi, uwazi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa jamii.
Kwa sasa, WMA ina ofisi katika mikoa yote ya Serikali Tanzania Bara kwa ajili ya kutoa huduma za uhakiki, ukaguzi na usimamizi wa matumizi sahihi ya vipimo.
Utekelezaji wa majukumu hayo unafanyika chini ya Sheria ya Vipimo Sura ya 340, inayoweka msingi wa usimamizi wa matumizi ya vipimo nchini.
Kwa kuendelea kuhakiki vipimo, kukagua maeneo ya biashara na bidhaa zilizofungashwa, WMA inalenga kuhakikisha mfumo wa upimaji nchini unalinda mlaji, unaongeza uaminifu katika biashara na kuwezesha ushindani wa haki katika shughuli za kiuchumi.




