Mheshimiwa Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amemwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, katika mazungumzo na Rais wa Mfuko wa Maendeleo wa OPEC, Dkt. Abdulhamid Alkhalifa, yaliyofanyika tarehe 16 Septemba 2026 katika Makao Makuu ya Mfuko huo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Kombo alimshukuru Dkt. Alkhalifa kwa kuidhinisha miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini Tanzania kupitia mikopo na misaada inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo wa OPEC.

Aidha, Balozi Kombo alithibitisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuendelea kushirikiana na Mfuko wa OPEC katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kipaumbele, ikiwemo nishati, hususan nishati safi ya kupikia, miundombinu ya usafirishaji, afya, elimu na kilimo.

Kwa upande wake, Dkt. Alkhalifa alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele.

Aidha, aliahidi kwa niaba ya Mfuko wa OPEC kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Mfuko huo, pamoja na kuifanya Tanzania kuwa kielelezo cha ushirikiano wa mfano barani Afrika.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kombo aliambatana na Mhe. Saada Salum Mkuya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb.), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia; Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati; Prof. Carolyne Nombo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; na Bw. Rished Bade, Kamishna wa Fedha za Nje kutoka Wizara ya Fedha.