Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema thamani ya mfuko huo imeongezeka na kufikia Shilingi trilioni 11.47, huku uwekezaji ukiongezeka kutoka Shilingi trilioni 4.6 Juni 2021 hadi zaidi ya Shilingi trilioni 9.6 Juni 2026.
Mshomba ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema ukuaji wa NSSF umeenda sambamba na ongezeko la malipo ya mafao kwa wanachama na wategemezi wao, ambapo mfuko huo ulilipa takribani Shilingi bilioni 594 katika kipindi cha mwanzo cha mpango uliopita, kabla ya kiasi hicho kuongezeka hadi zaidi ya Shilingi trilioni 1.16 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa idadi ya wanachama wanaofikia vigezo vya kupata mafao mbalimbali, ikiwemo pensheni ya uzeeni pamoja na mafao mengine yanayotolewa kwa mujibu wa sheria.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika mpango uliopita yameifanya NSSF kuendelea kuongeza idadi ya wanachama, makusanyo, uwekezaji pamoja na malipo ya mafao.
Mshomba amesema idadi ya wanachama iliongezeka kutoka 1,392,112 katika kipindi cha mwanzo cha mpango uliopita hadi zaidi ya milioni 2.1 kufikia Juni 2026.
Amesema ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, pamoja na hatua zilizochukuliwa na NSSF katika kuimarisha ukaguzi, uhusiano na waajiri na matumizi ya teknolojia.
Kwa upande wa makusanyo, Mshomba amesema NSSF ilikusanya zaidi ya Shilingi trilioni 1.17 katika mwaka wa mwanzo wa mpango huo, kabla ya kufikia Shilingi trilioni 2.90 katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema hatua hiyo inaonesha ongezeko kubwa la mapato yatokanayo na michango ya wanachama katika kipindi hicho.

Kuhusu ukusanyaji wa michango kutoka kwa waajiri, Mshomba amesema NSSF haitaogopa kumchukulia hatua mwajiri yeyote anayeshindwa kulipa michango kwa wakati, akieleza kuwa hatua ya mwisho ni kumfikisha mahakamani.
Amesema waajiri wanaofikishwa mahakamani wanatakiwa, kabla ya kesi kusikilizwa, kulipa asilimia 50 ya kiasi cha michango wanachodaiwa.
“Waajiri ni vema sasa wakaendelea na utaratibu wa kulipa michango kwa wakati ili kuondoa mivutano isiyokuwa na msingi na tutaendelea kusimamia sheria zetu ili kuhakikisha kila jambo linakaa katika mstari wake,” amesema Mshomba.
Mkurugenzi huyo amesema NSSF imejiwekea mikakati ya kuhakikisha ifikapo Juni 2031 thamani ya mfuko huo inafikia Shilingi trilioni 24.75, sambamba na kuongeza zaidi idadi ya wanachama.
Amesema mkakati huo pia unalenga kuimarisha uwezo wa Mfuko kifedha, ambapo thamani ya NSSF inatarajiwa kuongezeka kutoka Sh11.42 trilioni Juni 2026 hadi Sh24.75 trilioni Juni 2031, huku thamani ya uwekezaji ikipanda kutoka Sh9.61 trilioni hadi Sh20.35 trilioni. Aidha, Mfuko unalenga kukusanya michango yenye thamani ya Sh21.12 trilioni na kupata mapato ya uwekezaji ya Sh5.28 trilioni katika kipindi cha Julai 2026 hadi Juni 2031.





