Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Benki ya NMB kwa kushirikiana na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imewakutanisha vijana wabunifu 20 wenye utaalamu katika sayansi ya data, akili mnemba na sayansi ya kompyuta, ili kubuni suluhisho za kiteknolojia zitakazosaidia wakulima kupata huduma za kifedha na kuongeza tija.
AgriFin Hackathon 2026 inayofanyika Septemba 21–25 katika Kituo cha ICT cha NM-AIST, Arusha, inawapa washiriki nafasi ya kutumia maarifa yao kutatua changamoto halisi za sekta ya kilimo. Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu kutoka Makao Makuu ya NMB, Joanitha Rwegasira Mrengo, alisema mpango huo unaunganisha maarifa ya darasani na utengenezaji wa suluhisho zinazoweza kuwa na matumizi ya moja kwa moja kwa wakulima.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa NM-AIST anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Prof. Mwemezi Rwiza, alisema washiriki watapata mafunzo na ushauri katika akili mnemba, usalama wa mtandao na biashara ya kilimo, huku wataalamu wa NMB wakishiriki katika kutathmini na kuendeleza mifumo itakayobuniwa.
Hackathon hiyo itafungwa Septemba 25, ambapo washiriki watawasilisha suluhisho zao mbele ya majaji na washindi kutangazwa. Baadhi ya washindi wanatarajiwa kupata fursa za kuendeleza ubunifu wao nje ya Tanzania, ikiwemo Korea Kusini









