Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Korogwe
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amezindua rasmi mpango wa kupanga, kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Shamba la Mwakinyumbi lililopo Kata ya Hale, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga huku akiwataka wananchi wanaoishi eneo hilo kushirikiana na wataalamu ili zoezi hilo likamilike ndani ya muda uliopangwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika uwanja wa Mwenge, Hale Korogwe leo Sept 21, 2026 mkoani Tanga Mhe. Dkt Akwilapo amesema, hatua hiyo inalenga kuwatambua wananchi wanaostahili, kupangiwa na kupimiwa ardhi hiyo, na hatimaye kuwamilikisha viwanja vilivyopimwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Mpango wa uendelezaji wa ardhi katika eneo hilo unahusisha ekari 5000 zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kilimo, makazi na huduma za jamii, miundombinu, ardhi ya akiba, ardhi ya uwekezaji na uchimbaji madini, hifadhi ya mlima na hifadhi ya vyanzo vya maji. Aidha ekari 4,220 zimetengwa kwa vijiji vya Mwanyumbi Station na Miembeni na kufanya jumla ya ekari 9220 kuwa katika mpango huo wa uendelezajI.
Aidha, Dkt Akwilapo aliweka wazi kuwa, kabla ya kuanza kwa zoezi hilo la upangaji na upimaji, wananchi watapatiwa elimu kuhusu taratibu zitakazotumika, vigezo vya utambuzi, ukubwa wa maeneo watakayopangiwa pamoja na masuala mengine ya kisheria na kitaalamu.
” Niwaombe wananchi wa Mwakinyumbi kushiriki kikamilifu katika hatua hiyo ili kupata ufafanuzi na kuelewa namna zoezi litakavyotekelezwa”. Amesema
Mbunge wa jimbo la Korogwe Vijijini Mhe. Timotheo Mzava amemuomba Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha wananchi Mwakinyumbi katika kata ya Hale Korogwe wanapewa kipaumbele kwa kuwapatia viwanja kwa gharama nafuu.
Aidha, ametaka pasiwe na utaratibu wa kuwaondoa wanachi walioingia katika shamba la Mwakinyumbi na kufanya maendelezo kwa kuwa tayari wamefanya uwekezaji mkubwa.
” Pasiwe na utaratibu wa kuwaondoa wananchi wa Mwakinyumbi walifanya maendelezo na badala yake warasimishiwe maeneo yao kwa utaratibu ili waendelee kuishi”. Amesema Mhe Mzava
Eneo la mradi lilikuwa likimilikiwa na Kampuni ya M/S Mwakinyumbi iliyopewa ardhi hiyo mwaka 1989 kwa ajili ya uwekezaji katika kilimo cha mkonge. Hata hivyo, kampuni hiyo ilishindwa kutekeleza masharti ya umilikishwaji, ikiwemo kuliendeleza eneo hilo, hali iliyosababisha milki hiyo kubatilishwa mwaka 2023 na ardhi kurejea serikalini.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewaonya wananchi dhidi ya kuendelea kuuza au kununua ardhi kiholela katika eneo la Shamba la Mwakinyumbi wakati zoezi la upangaji na upimaji likiendelea.
Dkt Akwilapo amewataka wananchi wa eneo hilo kutoendeleza uvamizi wa ardhi au kufanya mauziano yasiyo rasmi, huku akianisha kuwa serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya baadhi ya watu wanaodaiwa kuuza ardhi kwa njia za ulaghai.









