Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

KAMPUNI ya Tanzania International Tourism Festival (TITF) imeandaa tamasha la Sanaa za ufundi litalalofanyika kuanzia tarehe 6 hadi 11 Oktoba jijini Arusha.

Tamasha hilo linalenga kuunganisha Sanaa, Ufundi, Utamaduni, Utalii na Uchumi wa Ubunifu, pamoja na kutoa fursa za masoko, biashara na uwekezaji kwa wazalishaji wa bidhaa za Sanaa na ufundi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Edward Buganga alisema TITF imezishirikisha BASATA, Bodi ya Filamu Tanzania na COSOTA katika maeneo yanayohusiana na majukumu yao.

Alisema tamasha hilo litafanyika katika Viwanja vya General Tyre, Njiro, Arusha.

Alisema BASATA itashiriki katika maeneo yanayohusu maendeleo na ukuzaji wa sanaa, wasanii na wadau wa sanaa, pamoja na kuhamasisha fursa zinazotokana na uchumi wa

ubunifu.

Buganga alisema Bodi ya Filamu Tanzania itashiriki katika maeneo yanayohusu tasnia ya filamu na namna filamu na Sanaa nyingine zinavyoweza kuunganishwa katika kukuza utamaduni, ubunifu na utalii.

Mkurugenzi Mtendaji wa TITF, Ibrahim Othman alisema tamasha linatarajiwa kuwa na zaidi ya washiriki 1,000, wakiwemo zaidi ya mafundi na waoneshaji 200, viongozi na watendaji wa Serikali, wawakilishi wa balozi na taasisi za kidiplomasia, wanunuzi wa kimataifa, wawekezaji, wadau wa utalii, uchumi wa ubunifu na vyombo vya habari.

Alisema tamasha hilo linabeba kaulimbiu “Crafted in Tanzania. Desired by the World.” inayolenga kuonesha ubora, ubunifu, thamani na upekee wa bidhaa za sanaa na ufundi zinazotengenezwa Tanzania, pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa masoko ya ndani na kimataifa.

Alisema lengo la tamasha hilo ni kuwa jukwaa la kuwaunganisha wazalishaji wa bidhaa za sanaa na ufundi, wasanii, wabunifu, wanunuzi, wawekezaji, wadau wa utalii, taasisi za Serikali na wananchi. Kupitia tamasha hili, mafundi na wabunifu watapata fursa ya kuonesha bidhaa zao, kujifunza, kutafuta masoko, kujenga mahusiano ya kibiashara na kupata fursa za uwekezaji.

Aidha, tamasha litaonesha mchango wa sanaa na ufundi katika ajira, biashara, uwekezaji, utalii wa kiutamaduni na maendeleo ya uchumi wa ubunifu.

Othmani alisema Tamasha litakuwa na maonesho ya teknolojia na ubunifu yanayolenga kuonesha matumizi ya teknolojia katika uzalishaji, kuongeza thamani ya bidhaa, masoko na maendeleo ya biashara za mafundi. Aidha, kutakuwa na ziara ya kujifunza katika Tanzania Engineering and Manufacturing Design Organisation (TEMDO).

Alisema kwa upande wa Sanaa na Utamaduni, kila jioni kutakuwa na maonesho ya Sanaa na

burudani, yakiwemo muziki, ngoma na Sanaa nyingine za maonesho.

“Pia kutakuwa na maonesho ya vyakula vya Kitanzania yatakayowawezesha wageni na wananchi kupata uzoefu wa aina mbalimbali za vyakula vya Tanzania,” alisema.