Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MANISPAA ya Kibaha imeweka mpango wa kujenga ofisi za walimu za kisasa katika kila shule, ikiwa ni hatua ya kuboresha mazingira ya kazi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ofisi zinazowakabili walimu.
Meya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, amesema hayo wakati akizungumza na wazazi, walezi, wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Kanesa, Kata ya Kongowe, akieleza kuwa ujenzi huo unalenga kuwajengea walimu mazingira salama na bora ya kufanyia kazi.
Dkt. Nicas amesema Manispaa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na wazazi katika kutatua changamoto za miundombinu ya elimu, akieleza kuwa tayari imeanza kuchukua hatua katika baadhi ya maeneo, ikiwemo upatikanaji wa madawati.
Ameelezea kuwa katika kukabiliana na changamoto ya uzio katika Shule ya Msingi Kanesa, wakuu wa shule wanapaswa kuhakikisha maeneo ya taasisi za umma, ikiwemo shule, yanarasimishwa na kupata hati ifikapo Februari 2027.
Ameeleza urasimishaji huo utasaidia kulinda maeneo ya taasisi za umma na kupunguza kero ya wananchi wanaozunguka maeneo hayo kuyamega, huku akieleza kuwa Manispaa imeanza zoezi hilo tangu mwaka 2025 na gharama ya urasimishaji ni shilingi 130,000.
Dkt. Nicas pia amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao na kuwa tayari kushindana katika soko la ajira, huku akiwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha watoto wanaendelea na elimu ya sekondari.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Africans Co. Ltd, Hafidh, amesema kampuni hiyo itapeleka samani kwa ajili ya Shule ya Msingi Kanesa pamoja na ofisi za walimu, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kanesa, Jordan Ngairo, amesema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni ukosefu wa uzio, hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi na mali za shule.
Amesema shule hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme, maji, vyoo vya walimu na darasa la awali, pamoja na upungufu wa samani, ambapo inahitaji viti na meza 96 kwa ajili ya ofisi za walimu.
Shule ya Msingi Kanesa imefanya mahafali yake ya tatu ikiwa na jumla ya wanafunzi 1,204, huku wanafunzi 129 wakiwa wahitimu.








