CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimezindua karakana maalumu ya uwekaji wa mfumo wa matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) kwenye magari, hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati hiyo na kujenga uwezo wa ndani katika teknolojia ya CNG.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Baraza la UDSM, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, amesema kituo hicho ni sehemu muhimu ya miundombinu ya Chuo na kinapaswa kusimamiwa kwa uwajibikaji ili kiendelee kutoa manufaa yaliyokusudiwa.

Amesema pamoja na uwekezaji katika vifaa na miundombinu, Chuo kinapaswa kuhakikisha karakana hiyo inatunzwa, inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kuendeshwa kwa kuzingatia viwango vya usalama.

Balozi Maajar pia amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa wataalamu wenye uwezo, mgawanyo wa majukumu na mfumo wa kufuatilia utendaji wa kituo hicho ili kuhakikisha kinatimiza malengo yake.

Ameeleza kuwa, matumizi ya CNG yana umuhimu mpana kwa Taifa, hususan katika kuongeza matumizi ya rasilimali za nishati zinazopatikana nchini na kujenga uwezo wa ndani katika teknolojia hiyo.

Amesema mwelekeo huo unaendana na Sera ya Taifa ya Gesi Asilia ya mwaka 2013, inayoweka msingi wa kuongeza matumizi ya gesi asilia katika uchumi wa ndani.

Ameongeza kuwa karakana hiyo haitapaswa kuonekana kama mradi wa Chuo pekee, bali pia kama sehemu ya kujenga utaalamu na uwezo wa Tanzania katika matumizi ya teknolojia ya CNG.

Balozi Maajar amewapongeza wataalamu na timu zilizoshiriki katika maandalizi ya karakana hiyo, huku akiishukuru Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ushirikiano na mchango wake katika kufanikisha kituo hicho.

Amesema Baraza la Chuo litaendelea kusimamia na kutoa mwelekeo ili kuhakikisha kituo hicho kinatumika ipasavyo, kinalindwa na kinatoa matokeo yanayotarajiwa kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo–Taaluma, Profesa Rose Upor, kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Anangisye, amesema uwekezaji huo utawezesha UDSM kuunganisha kwa karibu zaidi taaluma, utafiti na matumizi ya teknolojia katika mazingira halisi ya kazi.

Amesema karakana hiyo itatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo, huku watafiti wakitumia miundombinu hiyo kufanya tafiti za kuboresha teknolojia ya CNG, kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za matumizi yake.

“Uwekezaji huu utakuwa fursa muhimu kwa wanafunzi, watafiti na wataalamu kutumia taaluma katika kutatua changamoto halisi za sekta ya nishati na usafirishaji,” amesema Profesa Upor.

Ameongeza kuwa karakana hiyo pia inaendana na juhudi za UDSM katika kutekeleza masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), kwa kujenga uwezo wa watu na kukuza teknolojia yenye manufaa kwa jamii.