📍Yaeleza utekelezaji wa hoja za CAG kwa Mwaka 2024/25 na mikakati ya kuimarisha utendaji
Na Beatus Maganja, Dodoma
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewasilisha ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika kikao kilichofanyika Oktoba 7, 2026 Bungeni jijini Dodoma kikihusisha masuala ya uwajibikaji, udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu, utalii, uwekezaji na maendeleo ya jamii.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Beng’i Issa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko pamoja na Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, walifafanua masuala mbalimbali ya kimkakati yanayotekelezwa na Mamlaka kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji, kuimarisha uhifadhi, kukuza utalii, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo ya jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Kuhusu udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu, TAWA ilieleza kuwa imeongeza idadi ya ndege nyuki kutoka sita mwaka 2022 hadi 50 mwaka 2026, kuajiri askari 551 na kuongeza madaktari wa wanyamapori kutoka mmoja hadi watano. Aidha, wananchi 1,633,508 wamepatiwa elimu ya kujikinga na madhara yatokanayo na wanyamapori katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2026, huku Askari Wanyamapori wa Vijiji 187 wakishirikishwa katika wilaya 37 zenye changamoto kubwa za wanyamapori hao.
Kuhusu mpango wa uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas – SWICA), TAWA ilieleza kuwa mapato ya Mapori ya Akiba Ikorongo na Grumeti yameongezeka kutoka wastani wa Shilingi bilioni 1.9 hadi bilioni 9.25 kwa mwaka, huku mchango wa maendeleo kwa jamii ukiongezeka kutoka Shilingi milioni 26.24 hadi milioni 362.97 na kuwezesha upatikanaji wa madawati 3,014, kompyuta 21 na vitanda 24 vya wagonjwa.
Kwa upande wa Pori la Akiba Maswa, mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka wastani wa Shilingi bilioni 1.9 hadi bilioni 8.6 kwa mwaka, huku michango kwa jamii ikiongezeka kutoka Shilingi milioni 39.6 hadi bilioni 2.3, na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu, afya na miundombinu katika wilaya za Meatu, Bariadi na Itilima.
Katika kukuza utalii na kuongeza mapato, TAWA ilieleza mafanikio ya matumizi ya mfumo wa mnada wa kielektroniki wa vitalu vya uwindaji, huku mapato ya Mamlaka yakifikia Shilingi bilioni 87.32 katika mwaka wa fedha 2024/25. Aidha, Mamlaka imeweka mikakati ya kufikia mapato ya Shilingi bilioni 189 ifikapo mwaka 2027/28 kupitia uwekezaji, uboreshaji wa miundombinu na utangazaji wa vivutio vya utalii.
Akihitimisha kikao hicho, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Beng’i Issa, aliishukuru TAWA kwa ufafanuzi na majibu yaliyotolewa kuhusu masuala mbalimbali yaliyojadiliwa huku akitoa maelekezo yenye lengo la kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka.

















