Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia Bagamoyo
SERIKALI imewahakikishia wananchi wanaodai fidia baada ya kupisha eneo la mradi wa ujenzi wa Bandari ya Mbegani Bagamoyo, mkoani Pwani, kuwa inaendelea kuchukua hatua kulipa stahiki zao, huku taratibu za malipo zikiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, akiwataka wananchi kuwa na utulivu na kuendelea kuunga mkono ujenzi wa bandari hiyo inayolenga kuwa kituo cha kimkakati cha kuhudumia shehena zinazoingia na kutoka nchini.
Amesema utekelezaji wa Bandari ya Mbegani pamoja na uboreshaji wa Bandari ndogo ya Bagamoyo utafungua fursa kubwa za kiuchumi, ajira kwa vijana wa Wilaya ya Bagamoyo na kuongeza mapato ya Serikali.
Pia Bandari hiyo inalenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam, ambayo inaendelea kukaribia ukomo wa uwezo wa kuhudumia ongezeko la shehena na meli kubwa za kisasa.
Nyongo amesema Mbegani itakuwa kitovu mbadala kitakachosaidia kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena, kupunguza muda wa meli kusubiri nangani na kurahisisha usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bagamoyo, Subira Mgalu, ameeleza kuwa wananchi wamepata matumaini kutokana na uamuzi wa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Bandari ya Mbegani pamoja na maboresho ya Bandari ndogo ya Bagamoyo.
Mgalu amesema kwa sasa ushirikishwaji wa wananchi unaonekana, huku akieleza kuwa wana imani Serikali italipa fidia zinazodaiwa na wananchi waliopisha eneo la mradi.
“Licha ya wananchi kuahidiwa kulipwa fidia, pia walipewa ahadi ya kupewa maeneo, hivyo hili Serikali iliangalie kwa umuhimu wake,” amesisitiza Mgalu.
Naye Mkurugenzi wa Bagamoyo SEZ, Felix Michael, amesema katika tathmini iliyofanyika, jumla ya watu 1,154 wamelipwa fidia, huku watu 4,005.3 ambao tathmini yao ilifanyika miaka 16 iliyopita bado hawajalipwa na watu 1,130 hawajafanyiwa tathmini.
Amesema hali hiyo inafanya jumla ya watu 5,135 kuwa bado hawajalipwa fidia au hawajafanyiwa tathmini.
Kwa upande wake, Mhandisi Stephen John Mbogella, akimwakilisha Mkurugenzi wa Bandari, amesema Serikali imekamilisha uthamini na utwaaji wa eneo lote la mradi lenye ukubwa wa hekta 887, ambapo hekta 407 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya bandari na hekta 480 kwa ajili ya maeneo ya lojistiki na usafirishaji.
Amesema jumla ya Sh bilioni 49,007,851,429.84 zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo.
Mbogella amesema kwa sasa mchakato wa ununuzi unaendelea kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayefanya kazi ya kuchimba na kuongeza kina cha lango kuu la kuingilia meli pamoja na eneo la kugeuzia meli.
Amesema utekelezaji wa mradi umegawanywa katika awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa magati matatu yenye uwezo wa kuhudumia makasha 1,012,500 (TEUs) kwa mwaka, sawa na shehena yenye uzito wa tani 23,287,500.
Ameeleza kuwa shehena inayohudumiwa nchini imefikia zaidi ya tani milioni 30 mwaka 2026 na inatarajiwa kufikia zaidi ya tani milioni 50 ifikapo mwaka 2030, hali inayohitaji ujenzi wa miundombinu mipya na imara ya bandari.









