Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS), Richard Kayombo, amesisitiza umuhimu wa kuanza mapema maandalizi ya miundombinu ya shule za sekondari kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2028, kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari.

Akifunga mkutano wa uchaguzi mdogo wa kumchagua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT) wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kayombo amesema maandalizi ya madarasa na miundombinu mingine ya shule yanapaswa kupewa kipaumbele ili kukabiliana na mahitaji yatakayojitokeza mwaka huo.
Hatua hiyo inatokana na mpango wa kuwapokea wanafunzi wa Darasa la Sita na Darasa la Saba katika Kidato cha Kwanza kwa pamoja mwaka 2028, jambo linalohitaji maandalizi ya kutosha ya madarasa na huduma nyingine za shule ili kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi za kuendelea na masomo.

Aidha, Kayombo amewahimiza walimu wenye ulemavu kutoruhusu hali hiyo kuwakatisha tamaa katika kutekeleza majukumu yao, akisisitiza kuwa ulemavu haupaswi kuwa kikwazo cha kufikia malengo yao ya kitaaluma na kutoa mchango wao katika sekta ya elimu.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua kukabiliana na changamoto zinazowakabili walimu, ikiwemo kuongeza ajira, kupandisha madaraja na kulipa stahiki zao, huku akisisitiza umuhimu wa kufuatilia madai ya walimu ambao bado hawajapata haki zao.

Kayombo amesema walimu ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa kutokana na mchango wao katika kuandaa wataalamu na viongozi wa sekta mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kutambua nafasi yao na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao katika mazingira yanayowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

“CWT ni chama kikubwa kinachotambulika, na kundi hili la walimu ni hazina katika Taifa kwa kuwa lina nafasi kubwa katika kujenga Taifa kutokana na mchango wao katika kuzalisha wataalamu na viongozi kwenye sekta mbalimbali,” amefafanua Kayombo.

Pamoja na hayo, amewaelekeza maofisa elimu kuhakikisha walimu wanatendewa haki katika upandishaji wa madaraja kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa, akisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto zinazojitokeza ili kuimarisha ustawi wa walimu.

Vilevile, amewataka walimu kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, ili kuongeza uelewa na kuwasaidia kuchukua tahadhari zinazofaa wakati wa mvua hizo.

Kwa upande wake, Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Suzan Shesha, amesema mkutano huo uliandaliwa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa kumchagua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa (KUT), ambapo kura 37 zilipigwa. Mwita Magige aliibuka mshindi kwa kupata kura 20, huku Abdalrahmani Ahmadi akipata kura 16 na kura moja ikiharibika.

Shesha amesema Mkoa wa Pwani una jumla ya walimu 11,000, akimuomba Kayombo kusimamia uendeshaji wa mabaraza ya wafanyakazi kwa wakati ili kuimarisha mawasiliano, ushirikiano na utatuzi wa changamoto zinazowakabili walimu.

Kwa upande wake, Mwita Magige, aliyechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa, ameshukuru kwa ushindi alioupata na kuhimiza umoja na mshikamano miongoni mwa walimu, akiahidi kufikisha changamoto zao katika ngazi za juu ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.