Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imeeleza kuwa imekusanya Sh235.5 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026, kiasi kilichovuka lengo la Sh220 bilioni kwa asilimia 107 na kuwa kiwango cha juu zaidi cha makusanyo ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill M. Kiwia, amesema hayo jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 12, 2026, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa masomo 2022/2023 hadi 2026/2027.

Kiwia amesema kuanzia mwaka wa fedha 2005/2006 hadi Juni 2026, jumla ya Sh1.91 trilioni zilikuwa zimekusanywa kati ya Sh2.77 trilioni za mikopo iliyofikia muda wa kurejeshwa, sawa na ufanisi wa asilimia 69.

Alisema makusanyo yameendelea kuimarika, yakiongezeka kutoka takribani Sh177 bilioni mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh194 bilioni mwaka wa fedha 2024/2025, kabla ya kufikia kiwango cha Sh235.5 bilioni mwaka uliofuata.

Amesema mafanikio hayo yametokana na mikakati ya ukusanyaji wa madeni na ushirikiano na taasisi mbalimbali, huku HESLB ikiendelea na kampeni za #Fichua na #Kiduchu Fresh Tunasonga zinazolenga kuimarisha urejeshaji wa mikopo.

Kwa mujibu wa Kiwia, kampeni ya #Kiduchu Fresh Tunasonga, iliyozinduliwa Aprili 2026, inalenga kuwawezesha wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo yao kwa kiasi kinachoendana na uwezo wao.

Hata hivyo, alisema bado kuna changamoto ya kuwafikia baadhi ya wanufaika waliomaliza masomo, hususan wanaojishughulisha na shughuli za sekta isiyo rasmi.

Alibainisha kuwa takribani Sh800 bilioni zinadaiwa kutoka kwa wanufaika ambao bado hawajajitokeza kurejesha mikopo yao, hali inayohitaji kuimarishwa kwa mikakati ya ufuatiliaji na uhamasishaji.

“Mnufaika wa mkopo si mteja wa kawaida; yeye ni sehemu ya mnyororo wa uwezeshaji. Anaporejesha, fedha hizo zinaongeza fursa kwa kijana mwingine mhitaji kusoma,” amesema.

Alisisitiza kuwa uendelevu wa Mfuko unategemea ushirikiano wa wanufaika, waajiri na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha mikopo iliyotolewa inarejeshwa ili kuendeleza ufadhili wa vizazi vijavyo.

TEHAMA KUPUNGUZA USUMBUFU KWA WANAFUNZI

Kiwia amesema katika kipindi cha miaka mitano, HESLB imeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), ikilenga kurahisisha maombi, uchakataji wa mikopo, malipo na mawasiliano na wanafunzi.

Alitaja mifumo inayotumika kuwa ni pamoja na Mfumo wa Maombi na Usimamizi wa Mikopo kwa njia ya Mtandao (OLAMS), Akaunti Maalumu ya Mwombaji (SIPA), HESLB App na Mfumo wa Usimamizi wa Malipo ya Ada (DiDiS).

Alisema mifumo hiyo imesaidia kurahisisha baadhi ya taratibu, ikiwamo uhakiki wa taarifa za akaunti za benki, usajili wa wanufaika na uchakataji wa malipo ya ada.

Aidha, HESLB imeanza kutumia mifumo saidizi inayotumia akili unde, ikiwamo Bwanaboom na Bibiboom, kutoa majibu ya haraka kwa wanafunzi na wananchi wanaohitaji maelezo kuhusu huduma za mikopo.

Alisema lengo la maboresho hayo si kutumia teknolojia pekee, bali kuhakikisha huduma zinatolewa kwa haraka, kwa usahihi na kwa uwazi, huku taasisi ikiendelea kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko ya wateja.

Pamoja na hatua hizo, Kiwia alikiri kuwa bado kuna maeneo yanayohitaji kuimarishwa, ikiwamo mawasiliano na wanafunzi, usahihi wa taarifa zinazowasilishwa na waombaji pamoja na kukamilisha uunganishaji wa mifumo ya HESLB na vyuo.

Alivitaka vyuo na waombaji kuhakikisha wanawasilisha taarifa sahihi kwa wakati ili kurahisisha uchambuzi na upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa.