Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetenga rekodi ya Sh1.06 trilioni kwa ajili ya mikopo na ufadhili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026/2027, fedha zinazotarajiwa kunufaisha wanafunzi wasiopungua 300,000 wa vyuo vya elimu ya juu na vyuo vya kati.

Hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa uwekezaji katika elimu ya juu nchini, huku HESLB ikieleza kuwa mafanikio hayo yanaenda sambamba na mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa mikopo ili kuhakikisha fedha zinazoingia kwenye Mfuko zinaendelea kugharimia wanafunzi wengine wenye uhitaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill M. Kiwia, amesema hayo jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 12, 2026, wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa masomo 2022/2023 hadi 2026/2027.

Amesema bajeti ya mwaka huu imeongezeka kutoka Sh916.7 bilioni zilizotengwa mwaka wa masomo 2025/2026 na kunufaisha wanafunzi 289,932, sawa na ongezeko la takribani asilimia 15.6.

Kwa mujibu wa Kiwia, ongezeko hilo linaonesha dhamira ya Serikali ya kupanua fursa za elimu ya juu na kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata elimu na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maendeleo ya taifa.

“Tunapozungumzia mafanikio ya HESLB, hatuzungumzii fedha pekee. Tunazungumzia vijana waliopata nafasi ya kusoma, wahitimu walioingia katika soko la ajira, familia zilizopata fursa ya kubadilisha maisha yao na taifa lililoongeza uwekezaji katika rasilimali watu,” amesema.

Alisema katika Awamu ya Kwanza ya upangaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027, iliyotangazwa Oktoba 10, jumla ya wanafunzi 165,775 wamepangiwa mikopo na ruzuku zenye thamani ya Sh535.7 bilioni.

Kati yao, wanafunzi 74,769 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya Sh246.88 bilioni, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh22.9 bilioni.

Aidha, wanafunzi 873 wamepangiwa ruzuku kupitia programu ya Samia Scholarship zenye thamani ya Sh4.5 bilioni.

Kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, Kiwia amesema wanufaika 79,115 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo ya Sh252.4 bilioni, wanafunzi 1,554 wa stashahada wamepangiwa Sh3.8 bilioni, huku wanufaika 926 wa Samia Scholarship wakipangiwa ruzuku ya Sh5.1 bilioni.

Alisema HESLB inaendelea kupanua wigo wa ufadhili kwa kuzingatia mahitaji ya wanafunzi na vipaumbele vya maendeleo ya nchi, ikiwamo kuimarisha mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na programu maalumu zinazolenga taaluma muhimu kwa uchumi.

Katika mwaka wa masomo 2026/2027, wanafunzi 24,978 wanatarajiwa kufadhiliwa katika ngazi ya stashahada, wakiwamo wanafunzi wapya 14,000.

Kiwia alisema mikopo kwa wanafunzi wa ngazi hiyo ilianza mwaka wa masomo 2023/2024, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali za uzalishaji na ajira.

Aliongeza kuwa wanafunzi 2,738 wanatarajiwa kunufaika na Samia Scholarship katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), wakiwamo wanafunzi wapya 1,000.

Programu hiyo ilianzishwa mwaka wa masomo 2022/2023 kwa wanafunzi 636, huku mwaka wa masomo 2024/2025 HESLB ikipanua ufadhili huo kwa kuanzisha programu ya wanafunzi 80 wa shahada za uzamili.