*Gati jipya la mita 300, kina cha mita 13, laleta mapinduzi makubwa
*Mzigo wapanda kutoka tani 400,000 hadi tani milioni 2.6 ndani ya miaka mitano
*Malawi, Zambia, DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, Msumbiji zaitumia
Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Mtwara
Fumba na fumbua macho na kama umewahi kufika Mtwara rejea kumbukumbu ya picha ya zamani. Pia kama haujawahi kufika fanya rejea ya kumbukumbu ya simulizi za Mtwara ulizowahi kuzisikia kwa njia mbalimbali.
Kama kumbukumbu hizo bado unazo kichwani mwako anza kuzifuta kuanzia sasa kwa sababu Mtwara ya zamani uliyoisikia au kuiona imebadilika. Mtwara ya sasa ni tofauti. Shughuli za kiuchumi, biashara na uzalishaji zimeongezeka kwa kiwango kikubwa.
Kwa nini kuna ongezeko hilo? Jibu la swali hilo ni rahisi kabisa kwamba kuna maboresho makubwa ya kiutendaji, miundombinu na vifaa vya kisasa katika Bandari ya Mtwara yamefanyika. Kwamba maboresho hayo ndiyo yamesababisha hayo yanayoelezwa katika habari hii? Jibu ni ndiyo kwa sababu namba hazidanganyi.
Historia na mapinduzi ya miundombinu
Akizungumza katika mahojiano maalumu na JAMHURI ofisini kwake hivi karibuni, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema bandari hiyo ya kimkakati inasimamia shughuli za bandari ndogo za Kilwa Kivinje, Kilwa Masoko na Lindi zilizoko mkoani Lindi na bandari hiyo ni moyo wa uchumi wa nchi.
“Bandari hii ilijengwa miaka ya 1950 ikiwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka kwenye gati lenye urefu wa mita 385 na kina cha mita 9.5,” anasema.
Anasema kuna maboresho yamefanyika bandarini hapo ikiwamo ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na kina cha mita 13.
Mradi wa maboresho anasema umekamilika Desemba 31, 2020 kwa gharama ya Sh bilioni 157.8 na kutekelezwa na Kampuni ya CRMBEG na kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kufikia tani zaidi ya milioni mbili kwa mwaka kutoka tani 400,000 kwa mwaka.
Eneo lote la Bandari ya Mtwara, anasema lina jumla ya hekta 2,719 likijumuisha hekta 70 ilipo bandari ya sasa, hekta 25 kwenye vijiji vya Kisiwa na Mgao kunakoendelezwa bandari mpya ya kimkakati ya kuhudumia mzigo kwa wingi (bulk cargo) na eneo la hekta 2,624 zilizoko vijiji vya Ng’wale na Msangamkuu ambako kumetengwa kwa ajili ya mipango ya muda mrefu ya upanuzi wa shughuli za bandari.
Anasema bandari hiyo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji biashara kwenye ushoroba wa kusini, sasa inahudumia mizigo ya kimataifa (transit) kwenda nchi za Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Msumbiji.
“Wakati huo kabla ya maboresho tulihudumia zaidi mazao na korosho ndilo zao letu kubwa. Kipindi chote hicho hatukuwahi kufikia zaidi ya tani 400,000. Maboresho makubwa yamefanywa kwa kujenga gati kubwa. Tulipata gati nyingine kubwa tunayoiita mpya.
“Gati namba nne kwa sababu ile ya zamani ina namba moja, mbili na tatu. Hii mpya ni kubwa na ina uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na ilianza rasmi Desemba 30, 2020. Tangu kipindi hicho tumeona mabadiliko makubwa katika utendaji wa bandari,” anasema.
Tangu wameanza kutumia gati mbili (ya zamani na mpya) kwa wakati mmoja, anasema mizigo inaongezeka mwaka hadi mwaka.
“Kama umeona huko nyuma hatukuwahi kufikia mzigo wa tani 400,000 kwa mwaka. Baada ya gati mpya mzigo ukaongezeka hadi kufikia tani milioni mbili na mwaka hadi mwaka tunaongeza tani zetu kwa maana mizigo tunayosafirisha kupitia bandari hii.
“Ile gati ya zamani ina mita 385 lakini kina chake ni mita 9.5 sasa na kwa sababu imeendelea kutumika muda mrefu uko mpango wa kuongeza kina ili gati ya zamani iweze kuhudumia meli kubwa zaidi,” anasema.
Kwa sasa anasema uwezo wa bandari ni kuhudumia meli zenye urefu wa mita 245 huku wakiwa na maegesho ya urefu wa mita 385 na mita 300 za gati jipya na kufanya jumla maegesho yenye urefu wa mita 685.
KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 13-19, 2026



